Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mkazi wa Kisumu nchini Kenya, Victor Erick amewashangaza wengi baada ya kuibuka katika maandamano yaliyofanyika barabara ya Kisumu- Kakamega akiwa na mtoto wake wa kiume anayekadiriwa kuwa wa miaka mitatu huku wakiwa hawajavaa shati.
Mtandao wa Nation nchini Kenya umeripoti kuwa mwanaume huyo aliyeonekana akiwa amevaa skafu shingoni yenye bendera ya Kenya alikuwa amebeba bango lililoandikwa ujumbe kwa lugha ya Kingereza uliosomeka "Hatukati tamaa au kutafuta kumlazimisha Bw William Ruto apunguze Gharama ya Maisha, kuunda upya (Tume ya Uchaguzi) katika pande mbili na kuheshimu vyama vya kisiasa #Heshimu maoni ya Wakenya,"
Muandamanaji huyo amechukua huo wakati ambao, Rais William Ruto amesema hataruhusu kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga kutumia damu za Wakenya kujipatia madaraka huku akisema hawezi kuruhusu maandamano hayo kuendelea nchini humo huku Odinga akihamasisha wafuasi wa Kenya Kwanza kujitokeza kuandamana kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo wakiwa wamebeba sufuria.
Kuanzia asubuhi maofisa wa Polisi na vikosi vya kuzuia ghasia wamesambazwa maeneo mengi ya miji mikubwa nchini humo huku maduka yakifungwa kwa hofu ya uporaji kutoka kwa waandamanaji hao.
Wizara ya Elimu nchini humo pia ilitoa amri ya shughuli za masomo kwa wanafunzi wa kutwa kusitishwa kwa siku tatu ili kuwaepusha wanafunzi dhidi ya hatari ya kudhuriwa na waandamaji hao huku wadau wakidai wanafunzi hao watapoteza zaidi ya Saa 20 za vipindi shuleni.