STRAIKA wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ameshindwa kuficha hisia zake baada ya kutoka kuwa shujaa hadi kuwa wa hovyo dakika chache baada ya mchezo wa Europa kumalizika baina ya timu yake dhidi ya Olympiacos.
Arsenal walitupwa nje usiku wa jana katika mashindano ya Europa Ligi baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Emirates huku akishuhudiwa Aubameyang akipoteza nafasi ya wazi katika mchezo huo.
Mgabon huyo, alikuwa kwenye nafasi nzuri ya walau kuweka hai matumaini ya washika mitutu hao wa London kusonga mbele muda mchache kabla ya mchezo kumalizika, lakini akajikuta akipoteza nafasi hiyo ya wazi.
Baada ya kupoteza nafasi hiyo, Aubameyang alionekana kuziba uso wake kama ishara ya kujutia kilichotokea huku ukimya ukitawala kwa mashabiki wa Arsenal waliojitokeza kwenye mchezo huo.
"Nimehuzunika na kilichotokea hicho ndicho ninachoweza kusema. Ni ngumu na imenigusa," alisema Aubameyang.
Aliongeza kwa kusema, "Nadhani tulipoteana hilo limetugharimu katika huu mchezo, hatukuwa na bahati. Kilichopo ni kujaribu kuhamishia nguvu zetu kwenye ligi."
Youssef El-Arabi ndiye aliyezamisha jahazi la Arsenal katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kufunga bao la pili kwa Olympiacos dakika ya 120, ndani ya dakika 90 za kawaida washika mitutu wa London walifungwa bao moja hivyo ilibidi wakaamuliwe dakika 30 kwani mchezo wa kwanza, walishinda bao 1-0 nchini Ugiriki.
Aubameyang, ambaye mchezo huo alifunga bao la kufutia machozi kwa Arsenal licha ya kupoteza nafasi ya wazi, msimu uliopita alitwaa tuzo ya kuwa mfungaji bora wa msimu wa Ligi Kuu England 'EPL' na Mohamed Salah na Sadio Mane wa Liverpool kila mmoja akipachika mabao 22.