Muhammadu Ali (43), ameuawa kwa kupigwa risasi katika jimbo la Bauchi Kaskazini Mashariki, nchini Nigeria kwa kile kinachodaiwa kuwa majaribio kama hirizi ya kuzuia risasi - au "dawa ya bunduki" inafanya kazi.
BBC imeripoti kuwa majaribio hayo yalikuwa yakifanywa na mganga wa kienyeji kwa mujibu wa Msemaji wa Polisi eneo hilo, Ahmed Wakil.
Mganga huyo ambaye anadaiwa kufyatua risasi hiyo kwa kutumia bunduki iliyotengenezwa kienyeji, amekamatwa, pamoja na watuhumiwa wengine wawili, huku wengine hawajulikani walipo baada ya kutoroka.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Polisi walifika eneo la tukio mara tu waliposikia kuhusu ufyatuaji wa risasi, na kumpeleka Ali hospitalini, hata hivyo, alitangazwa kuwa amefariki mara tu alipofikishwa.
Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika, amesema Wakil.
Inadaiwa kuwa hirizi zinazoaminika kuwa na nguvu za kishirikina hutumiwa sana nchini Nigeria, ambapo watu wengi huwasiliana na waganga wa kienyeji kuhusu masuala mbalimbali.
Lakini kumekuwa na ripoti kadhaa za watu kuuawa baada ya kujaribu kile kinachoitwa hirizi zinazozuia risasi.