Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari wa SADC waingia DRC kukabiliana na waasi

SADC Waingia DRC Askari wa SADC waingia DRC kukabiliana na waasi

Sat, 30 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamia ya wanajeshi wa Afrika Kusini wamewasili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakiwa ni sehemu ya vikosi vya kijeshi vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambavyo vitakabiliana na waasi katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Wanajeshi wa hao wa SADC ambao watasaidiana na jeshi la serikali, FARDC kujibu mashambulizi kutoka kwa vikundi vilivyojihami mashariki mwa nchi hiyo, wameshawasili huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Taarifa za Ijumaa zinasema kikosi hicho cha kwanza kiliwasili usiku wa Desemba 26 na kuwasili kwao kunafuatia makubaliano kati ya SADC na DRC yaliyotiwa saini na Rais Felix Tshisekedi na jumuiya hiyo tarehe 17 mwezi uliopita wa Novemba kwenye mji mkuu Kinshasa.

Wakuu wa SADC walipokutana Luanda, Angola tarehe 4 mwezi uliopita wa Novemba walijadili hali ya Usalama Mashariki mwa DRC tangu kuibuka tena mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23 na kukubaliana uwezekano wa kutuma jeshi la kikanda kuchukua nafasi ya lile la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo muda wake ulipomalizika Desemba 8.

Tarehe 11 mwezi huu wa Desemba wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita alisema, "hatua hizi za kikanda ni za kupongezwa."

Kupelekwa kikosi hicho cha SADC ni kwa mujibu wa Ibara ya 6, kifungu cha 1 cha Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa jumuiya hiyo unaosema, shambulio la kijeshi dhidi ya mwanachama wa jumuiya litachukuliwa kama tishio la ulinzi na usalama. Hivyo kujibu shambulio hilo kutalazimu hatua za pamoja zichukuliwe.

Mwezi Oktoba mwaka huu, msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya aliziambia duru za habari kwamba, serikali ya nchi hiyo haingewapatia kandarasi mpya wanajeshi hao wa kieneo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

DRC ilitangaza msimamo huo baada ya muungano wa vyama vya kiraia nchini Kongo DR kufanya maandamano mjini Goma ukitaka kikosi hicho cha pamoja cha Afrika Mashariki kuondoka mashariki mwa nchi hiyo, kutokana na kushindwa kukabiliana na waasi wa M23.

Eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na mizozo na mapigano kwa takriban miaka 30 sasa, kutokana na harakati za makundi ya waasi wenye kubeba silaha, ya ndani na nje ya nchi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live