Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari apokonywa Bastola na majambazo

Bastola Askari apokonywa Bastola na majambazo

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: globalpublishers.co.tz

Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamempora bastola yenye risasi kumi na tano afisa wa polisi, George Kingi Bamba, jirani na kivuko cha Likoni, Mombasa nchini Kenya.

Akisimulia tukio hilo, Kamishna wa Polisi wa Jiji la Mombasa, Manaseh Musyoka amesema tukio hilo limetokea usiku wa Jumatatu, majira ya saa nne na dakika ishirini za usiku, ambapo afisa huyo wa polisi alikuwa akiendesha gari lake binafsi akielekea nyumbani kwake ambapo ghafla, pikipiki iliyokuwa imebeba watu watatu ilimpita na kusimama katikati ya barabara.

Ameongeza kuwa, kitendo hicho kilimfanya askari huyo asimamishe gari lake kutaka kujua kinachoendelea ambapo ghafla, alivamiwa na majambazi hao ambapo mmoja alimnyooshea bastola na kumtaka ajisalimishe.

Baada ya kujisalimisha, watu hao walimpekua na kuchukua bastola aliyokuwa nayo kiunoni mwake na kutimua mbio kwa kutumia pikipiki hiyo, kuelekea kwenye Kivuko cha Likoni.

Muda mfupi baada ya majambazi hao kukimbia, askari huyo alitoa taarifa kwa wenzake ambapo msako mkali ulianza muda huohuo bila mafanikio.

Kamanda Musyoka amesema bado jitihada za kuitafuta silaha hiyo na wahusika wa tukio hilo zinaendelea na kuwataka wakazi wa Mombasa kutoa ushirikiano kwa polisi ili kuwapata wahalifu hao.

Chanzo: globalpublishers.co.tz