Mwanaume mmoja aliyefanyiwa uchunguzi na BBC Africa Eye amepatikana na hatia ya kusafirisha walemavu nchini Kenya, na kupewa amri ya kulipa faini ya shilingi 30,000,000 za Kenya sawa na $242,000 au £196,000 au afungwe miaka 30 gerezani.
Mwezi Juni mwaka jana, uchunguzi wa siri wa BBC ulifichua mtandao wa magendo ya binadamu unaosafirisha watoto walemavu kutoka Tanzania hadi Kenya.
Wengi walichukuliwa kutoka kwa wazazi wao kwa ahadi ya maisha bora.
Badala yake, watoto walilazimishwa kuomba mitaani - kwa miaka mingi- wakati watekaji wao wakichukua faida zote.
Baadhi ya waathiriwa walidai walipigwa ikiwa hawakupata pesa za kutosha.
James Zengo Nestory alikamatwa na sasa amehukumiwa na mahakama katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
“Pia nimebaini kuwa wewe ni mlemavu. Gereza huenda lisiwe mazingira mazuri kwako,” alisema hakimu Agnes Wahito.
"Hili ni kosa lako la kwanza hivyo nimekupa adhabu ya chini ya kulipa shilingi 30,000,000 za Kenya. Usipokuwa nazo utafungwa jela miaka 30.