SERIKALI ya Angola imesema inazungumza na serikali ya Tanzania ili kuunganisha reli ya moja kwa moja kati ya Bandari ya Dar es Salaam na ile ya Lobito nchini Angola ili kurahisisha usafirishaji mizigo na kutengeneza fursa za ajira.
Balozi wa Angola nchini, Sandro De Oliveira alisema Tanzania ni moja ya nchi rafiki zilizosaidia taifa hilo kwenye harakati za ukombozi na kwamba uhusiano wa kidiplomasia umeimarika na ndio sababu wanataka kuuendeleza kwa kuunganisha reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya Uhuru wa Angola.
“Tuna uhusiano nzuri na Tanzania tangu harakati za uhuru na sasa baada ya uhuru tumeendelea kuwa pamoja na katika kukuza uchumi wa mataifa yetu na watu wetu ndio maana tumedhamiria kuunganisha reli baina ya miji hiyo miwili yenye bandari kubwa za kibiashara,"alisema Balozi De Oliveira.
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na kubainisha fursa za uwekezaji nchini humo kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Balozi De Oliveira alisema pamoja na nchi hizo kuwa na uhusiano mzuri kiwango cha biashara baina yao bado kiko chini kutokana na changamoto za miundombinu.
"Pamoja na kuwa tuna uhusiano nzui na Tanzania bado kiwango cha biashara baina yetu ni kidogo, wananchi wa mataifa haya mawili hawajafaidika sana na uhusiano huu ndio sababu tumeweka mazingira bora ya kufanya biashara na watu kusafiri na iwapo hili la reli litafanikiwa tutafungua ukurasa mpya wa kufanya biashara," alisema Balozi De Oliveira .
Mshauri wa Masuala ya Biashara wa Ubalozi wa Angola, Ngueza Mauricio alisema Angola imepakana na Zambia ambayo ina reli kutoka Zambia hadi Tanzania.
Maurcio alisema changamoto iliyopo ilikuwa ni kubadilisha aina ya reli kutoka Angola kwenda Zambia ili iweze kufanana na hiyo reli ya Taraza na kwamba mazungumzo baina ya Tanzania na Angola kuhusiana na hilo yanafanywa ili kuunganisha miji hiyo ya kibiashara.
"Tunataka kuunganisha miji yetu, Lobito na Dar es Salaam ambayo pia kila moja ina bandari kubwa zinazofanya biashara, sasa tukifanikiwa kuziunganisha, biashara itakuwa nzuri, fursa za ajira zitafunguka, usafiri wa migizo na bidhaa utarahisishwa na uchumi wa mataifa yetu utakuwa, lakini kubwa zaidi tutaunganisha usafiri kwenye bahari ya Hindi na ile ya Atlantic," alisema Mauricio.