Mchungaji wa Kanisa la Good News International, Paul Mackenzie amejisalimisha polisi mjini Malindi, Kenya baada ya taarifa kusambaa mitandaoni kuwa anasakwa na polisi na atafikishwa mahakamani wiki ijayo.
Alhamisi Februari 13, 2023 polisi walifanya msako eneo la Shakahola ambapo wasamalia wema walitoa taarifa uwepo wa watu waliofunga mfululizo ili wakutane na Yesu ambapo 15 walikutwa wamedhoofika na wanne walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu.
Mmoja wa waliookolewa amesema alimjua mchungaji huyo kupitia kituo cha televisheni cha Times kinachoonesha mahubiri ya Mackenzie.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ijumaa Aprili 14, 2023 katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi anakoendelea kupata matibabu, Wycliffe Timbo (43) amesema alianza kusali katika kanisa hilo baada ya kuvutiwa na mahubiri ya mchungaji huyo.
“Nilikuwa nikitazama runinga ya Border TV lakini mwaka 2017 nilipoanza kutazama runinga ya Times TV nilivutiwa sana na mafundisho ya mchungaji Mackenzie,” amesema Timbo.
Timbo amesema baada ya mchungaji huyo kufunga kanisa hilo pamoja na kituo cha runinga ya Times TV, yeye alianza kujihusisha na kilimo cha mahindi, maharage na mbogamboga.
Alhamisi iliyopita alifikishwa katika hospitali ya Malindi akiwa na hali mbaya akiwa hajala chochote kwa siku 21 baada ya kufunga ili afariki dunia na kukutana na Yesu Kristo.
“Hivi unavyoniona hapa nikija kuchukuliwa kule Shakahola na kuletwa hapa nilikuwa na zaidi ya siku 21 nimefunga sili wala sinywi chochote. Na hii iko katika kitabu cha Warumi…, Biblia inasema itoeni miili yenu kama dhabihu…, mimi nilikuwa nimejitolea kufa ili niweze kuurithi uzima wa milele,” amesema Timbo.
Amebainisha kuwa kuna baadhi ya watu wamepoteza maisha eneo hilo lakini hawezi kujua idadi kamili na wala hajui mahali walipozikwa.
“Siwezi kusema hakujakuwa na maafa maana yapo ila sio kwamba walikufa kwa sababu walilazimishwa kufunga na mchungaji. Walijitolea wenyewe kufanya hivyo ili waweze kuurithi ufalme wa mbinguni," amesema Tambo akisisitiza bado anayapenda mafundisho ya mchungaji huyo na akipona ataendelea na imani hiyo.
Akithibitisha kujisalimisha kwa Mackenzie, ofisa mkuu wa upelelezi wa jinai, Charles Kamau amesema kwa sasa mchungaji huyo anashikiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu ijayo.