Algeria imetangaza kusitisha juhudi zake za kupatanisha mgogoro wa kisiasa nchini Niger kufuatia mapinduzi ya mwezi Julai.
Wizara yake ya mambo ya nje ilisema katika taarifa yake Jumatatu kwamba matamko kutoka kwa mamlaka ya Niger yameibua "maswali halali kuhusu nia yao ya kweli ya kufuata kukubali kwao upatanishi wa Algeria".
Sasa imesimamisha mchakato huo ikisubiri kujitolea kutoka kwa junta kuendelea na upatanishi.
Mwezi uliopita, Niger ilikubali pendekezo la Algeria la kuwa mpatanishi katika mgogoro wake wa kisiasa unaolenga kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kikatiba.
Mwezi Agosti, Algeria ilipendekeza kipindi cha mpito cha miezi sita kikiongozwa na mamlaka ya kiraia.
Lakini mkuu wa junta, Jenerali Abdourahamane Tchiani, ambaye alichukua mamlaka mwezi Julai, alitaka kipindi cha mpito cha miaka mitatu.
Algeria pia ilipinga suluhu la kijeshi kwa mzozo wa Niger kufuatia vitisho vya Ecowas kuhusu uwezekano wa kuingilia kijeshi kurejesha demokrasia.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa shirikisho hilo la kikanda alikafiki mchakato wa upatanishi, lakini uamuzi huu wa Algeria utavuruga zaidi juhudi za kutatua mzozo wa kisiasa nchini Niger.