Mamlaka katika mataifa ya Algeria na Morocco zimeimarisha kiwango cha tahadhari katika mipaka yake ili kupunguza uwezekano wa kuenea kwa kunguni wa Ufaransa ambao wanaitesa nchi hiyo kwa sasa.
Taarifa kutoka wizara za afya za mataifa hayo zilisema kuwa zinaanzisha ufuatiliaji wa afya kwa kuua vijidudu kwa ndege, meli na magari katika sehemu za kuingilia kutoka mataifa ya nje.
Hatua hizo zinatokana na hofu iliyotanda nchini Algeria na Morocco kwamba wadudu hao wanaonyonya damu wanaweza kuingia kutokana na idadi kubwa ya watu wanaosafiri kati ya nchi hizo na Ufaransa.
Nchini Morocco, serikali imetangaza kuchukua hatua kama ilizochukua jirani yake Algeria kama sehemu ya mikakati ya kuzuia kusambaa kwa wadudu hao katika eneo lake.
Wakati huo huo Waziri wa Elimu wa Ufaransa, Gabriel Attal ametangaza kufungwa shule saba zinazowapokea wanafunzi wapatao 1,500 baada ya kuvamiwa na kunguni.
Awali shule zilizofungwa zilikuwa mbili kutoka katika miji ya Marseille na nyingine Villefranche-sur-Saone nje kidogo ya mji wa Kusini Mashariki wa Lyon.
Serikali ya Ufaransa imefanya mikutano mingi wiki hii kuchunguza ongezeko la kunguni wakati taifa hilo likiandaa Kombe la Dunia la Rugby na itakuwa mwenyeji ya Michezo ya Olimpiki mwaka ujao.
Waziri wa Usafiri, Clement Beaune alikutana na makampuni ya usafirishaji kubuni mpango wa kufuatilia na kunyunyizia dawa vyombo vya usafiri wa umma na kujaribu kupunguza wasiwasi wa nchi nzima uliochochewa zaidi na vyombo vya habari.