Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alazimika kusalia katika choo cha ndege kwa saa tano baada ya kukutwa na corona

Covid Ndege Alalazimika kusalia katika choo cha ndege kwa saa tano baada ya kukutwa na corona

Fri, 31 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwalimu mmoja wa shule nchini Marekani anasema alitumia saa tano kujitenga kwa hiari kwenye choo cha ndege baada ya kupimwa na kukutwa na Covid-19 katikati ya safari ya ndege.

Marisa Fotieo anasema alihisi koo lake likimuuma alipokuwa akisafiri kutoka Chicago kwenda Reykjavik, Iceland, tarehe 20 Desemba.

Bi Fotieo anasema alifanya kipimo cha haraka kwa kifaa alichokuja nacho, ambacho kilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa.

Alibaki chooni kwa muda wote uliosalia wa safari, na mtumishi wa ndege alimpa chakula na vinywaji.

Haikuwa wazi mara moja ikiwa alilazimika kuwasilisha kipimo cha Covid-19 kabla ya kupanda ndege.

"Ilikuwa tukio la kichaa," Bi Fotieo, ambaye anatoka Michigan, aliambia NBC News. "[Kulikuwa na] watu 150 kwenye ndege, na hofu yangu kubwa ilikuwa kuwaambukiza".

Video aliyochapisha kwenye Tiktok akiwa ndani ya choo cha ndege ya Icelandair imetazamwa zaidi ya mara milioni nne. Alimsifu mhudumu wa ndege kwa kumsaidia wakati wa tukio hilo

"Alihakikisha kuwa nina kila kitu nilichohitaji kwa saa tano zilizofuata kutoka kwa chakula hadi vinywaji na mara kwa mara aliniangalia na kunihakikishia kuwa nitakuwa sawa," aliiambia NBC.

Bi Fotieo alisema ilimbidi kujitenga katika hoteli ya Msalaba Mwekundu alipowasili Iceland.

Masaibu yake yalikuja huku kukiwa na kuenea kwa aina ya Omicron ya Covid-19, ambayo inaendelea kuchochea kuongezeka kwa kesi kote Marekani. Uchunguzi unaonyesha aina hii ya virusi ni dhaifu kuliko zingine lakini inaambukiza kwa kasi.

Kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani wastani wa siku saba wa kesi mpya ni 277,000 nchini, kiwango cha juu zaidi tangu kuanza kwa janga hilo. Viwango vya vifo na kulazwa hospitalini, hata hivyo, vinaendelea kuwa sawa.

Idadi inayoongezeka ya watu wanaolazimika kujitenga kwa sababu ya maambukizo imeweka shinikizo kwa tasnia kadhaa, pamoja na usafiri wa anga. Usumbufu uliendelea kwa siku ya sita siku ya Alhamisi, na takriban safari 1,100 zikisitishwa kote nchini, kulingana na tovuti ya data ya safari za ndege ya FlightAware.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live