Kundi la wanamgambo la al-Shabab limedai kuwaua wanajeshi tisa wa Uganda mnamo tarehe 15 Aprili, katika shambulizi la kuvizia katika eneo la kusini mwa Somalia la Lower Shabelle, msemaji wa kundi hilo aliripotiwa katika Radio Andalus jana.
Wanajeshi wengine nane wa Uganda waliripotiwa kujeruhiwa katika shambulizi hilo, ambalo lilizua mapigano makali ya saa kadhaa kwenye viunga vya mji wa Janale.Vilevile, Wanamgambo hao pia waliharibu magari manne ya kijeshi katika mapigano hayo, ilisema redio hiyo.
Uganda ina zaidi ya wanajeshi 6,000 walinda amani wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia, ambao wamekuwa wakiunga mkono serikali ya shirikisho iliyo dhaifu mjini Mogadishu tangu mwaka 2007.
Ni mara chache Uganda na ujumbe wa AU inatoa maoni yoyote kuhusu hasara iliyotokea wakati wa operesheni za kukabiliana na waasi nchini Somalia.