Vikosi Maalumu vya Danab vya jeshi la Somalia vimeua makumi ya magaidi wa al-Shabaab katika operesheni ya hivi punde katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Magaidi hao wameangamizwa saa chache kabla ya vikosi vya Somalia kuanza operesheni nyingine dhidi ya kundi hilo katika majimbo ya Jubaland na Kusini Magharibi.
Wimbi la operesheni hizi limekuja baada ya wanajeshi kadhaa wa Jeshi la Taifa la Somalia kuuawa na wanachama wa al-Shabaab katika kijiji cha Oswein, katikati ya nchi.
Arab Dheeq Ahmed, Kamanda wa Kikosi cha 5 cha Vikosi vya Danab amesema magaidi zaidi a 47 wa al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni hiyo mpya iliyolenga maficho yao katika eneo la Yaq Dabey, jimbo la Lower Juba. Wanajeshi wa Somalia
Amesema, "Makomandoo wa Kikosi cha 5 cha Danab wamefanya operesheni za kusafisha katika jimbo la Lower Juba ili kuwatimua wahalifu waliokuwa wamejificha katika msitu ulioko katika eneo hilo."
Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, magaidi zaidi ya 3,000 wameuawa katika awamu ya kwanza ya operesheni za kulitokomeza kundi hilo hasa katika majimbo la Hirshabelle na Galmadug.
Hivi karibuni, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alisema lengo la operesheni za kijeshi zinazoendelea nchini humo ni kulitokomeza na kulisambaratisha kundi la kigaidi la al-Shabaab katika kipindi cha miezi mitano ijayo.