Jeshi la Somalia limetangaza kuwa limeangamiza zaidi ya magaidi 30 wa al-Shabab katika operesheni iliyofanyika katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii ya Somalia imetangaza habari hiyo mjini Mogadishu na kusema: "Operesheni hiyo imeangamiza magaidi 30 wa al Shabab, kuharibiwa magari manne na kukamatwa magari mengine mawili pamoja na silaha,"
Taarifa hiyo imeongeza kwa kuksema: "Tunawashukuru raia majasiri waliochagua kusimama pamoja na Serikali dhidi ya adui. Tumeungana katika dhamira yetu ya kulitokomeza kundi la al-Shabab."
Wizara hiyo pia imethibitisha kuwa Mohamed Bashir Muse, kiongozi mkuu wa genge la al-Shabab, ni miongoni mwa magaidi 30 walioangamizwa kwenye operesheni hizo.
Taarifa ya wizara hiyo imesema, operesheni za pamoja za kijeshi zinaendelea katika maeneo yaliyoko chini ya wilaya ya Mahaday katika eneo la Shabelle ya Kati na zinawalenga magaidi wa ngazi za juu wa genge la al-Shabab waliojificha karibu na kingo za mito. Wanajeshi wa Somalia
Wananchi wa kawaida wanaokaa maeneo hayo wanasema, vikosi vya jeshi la Serikali kwa kushirikiana na vikosi vya eneo hilo vimechukua udhibiti kamili wa vijiji vya Sargo na Qodqod vya mkoa wa Mudug.
Hatua hiyo imekuja wakati Ujumbe wa Mpito wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kupunguza wanajeshi wake mwezi huu ambapo wanajeshi wengine 3,000 wa kikosi hicho watapunguzwa baada ya kufanikiwa kuwaondoa wanajeshi 2,000 na kukabidhi kambi sita za kijeshi kwa askari wa serikali ya Somalia mwezi Juni mwaka huu. Kupunguzwa wanajeshi 3,000 wa AU katika awamu ya pili kunatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.