MSHAMBULIAJI Walter Bwalya aliyekuwa akikipiga katika timu ya Nkana FC ya Zambia amejiunga rasmi na klabu ya Al Ahly ya Misri, imeelezwa.
Nyota huyo alikuwa katika rada za mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba wakimtaka kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi hicho, ametua Al Ahly akitokea timu nyingine ya nchini humo ya El Gouna.
Hatahivyo, mitandao mbalimbali ya Misri ukiwemo ule wa kingfut.com ulithibitisha jana kuwa mchezaji huyo ametua katika klabu ya Al Ahly kwa mkataba wa miaka minne akitokea klabu ya nchini humo ya El Gouna, ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Misri.
Baada ya kumalizana na Nkana, Bwalya mwenye umri wa miaka 25, aliibukia katika klabu ya El Gouna, ambako aliifungia timu hiyo mabao 16 tangu alipowasili Misri Julai mwaka 2019 akitokea Nkana, na kucheza mechi 34.
Hatua hiyo ya timu hiyo kumsajili mchezaji huyo imekuja baada ya kukwama kumsajili mshambuliaji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Gastón Sirino.
Msimu uliopita mchezaji huyo alifunga mabao 13 katika mechi 30 na kuisaidia timu hiyo kukwepa kushuka daraja, kabla ya kufunga matatu katikamechi tano alizocheza msimu huu wakati El-Gouna ikikalia kiti cha msimamo wa Ligi Kuu ya Misri.