Joshua Odoyo Nyariera, mwenye umri wa miaka 23, anaripotiwa kujitoa uhai katika Kanisa la Oneno Nam Raha Msalaba, siku ya Jumamosi, Januari 8, dakika chache baada ya waumini wa kanisa hilo kuanza ibada ya Sabato.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, Odoyo aliwacha nyuma kijikaratasi akisema kuwa aliamua kujiua sababu ya kulemewa na madeni aliyoshindwa kulipa.
Marehemu ambaye alikuwa mhudumu wa Mpesa mjini Homa Bay, pia aliongeza kuwa alihofia kukamatwa na polisi na kusukumwa jela ilhali hangeliweza kumudu gharama ya wakili wa kumwakilisha kortini.
Kulingana na mzee wa kanisa hilo, Benson Oyieng, marehemu alikuwa akiabudu nje ya kanisa kabla ya tukio hilo.
Awacha masharti makali ya namna atazikwaOyieng alisema Odoyo pia alitoa maagizo ya namna alitaka mazishi yake yaandaliwe, akiamuru kuwa mwili wake kamwe usihifadhiwe mochari akitaka uteketezwe na kisha majivu yazikwe.
Mzee huyo aliwaomba waumini wa kanisa hilo kufunguka kuhusu changamoto zao kwa wenzao badala ya kujiua.
Katika tukio tofauti polisi wamemtia nguvuni mwanamume mwenye umri wa miaka 38 baada ya kuhusishwa na mauaji ya mkewe na watoto wao watatu huko Elburgon, kaunti ya Nakuru.
Inadaiwa kuwa mwanamume huyo aliwaua wanne hao kabla ya kuteketeza nyumba yao kufuatia mzozo wa kinyumbani unaoshukiwa kuchangia kisa hicho.
Wenyeji walisema walimsikia mwanamume huyo akiwaomba majirani kumsaidia kuzima moto huo.
Naibu kamishna wa kaunti ya Molo Josphat Mutisya alithibitisha kisa hicho na kusema jamaa huyo kwa sasa yuko mikononi mwa polisi akiwasaidia kufanya uchunguzi.