Mzee Samuel Maikut (6O) amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kwenda kwenye sherehe ya utambulisho na kutoa mahari akiwa mikono mitupu.
Mzee Maikut ambaye ni mkazi wa Jimbo la Kitawoi, Wilaya ya Kween nchini Uganda, imeelezwa kwamba aliwasili nyumbani kwa wakwe zake wilaya ya Bukwo mwishoni mwa wiki iliyopita saa 11: 30 jioni akiwa mikono mitupu.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa The Monitor wa Uganda, imeeleza kuwa baba wa binti anayetakiwa kutolewa mahari, Christopher Ngania alisema ni jambo lisilokubalika kuwapokea wageni kwenye sherehe ya kutoa mahari wakiwa mikono mitupu.
“Tulikubaliana kwamba muoaji na timu yake wangekuja na ng'ombe wanne, mbuzi watatu, lakini badala yake wamekuja mikono mitupu,” amesema Ngania ambaye ni baba mzazi wa bibi harusi mtarajiwa.
Ngania amesema awali hakutaka kumkomoa muoaji bali aliamua mwenyewe kuwa zifanyike sherehe mbili pamoja na ile ya utambulisho, lakini amekwenda kinyume na makubaliano.
Awali, tulikubaliana sherehe ingefanyika Desemba 2, 2023 na tulimkaribisha kwenye familia Novemba 30 na kumshauri afanye sherehe moja , akasisitiza sherehe zitafanyika mbili.
“Tulikaa kuwasubiri wageni wetu, nasi tuliwaruhusu wageni wa upande wetu waanze kula na kunywa. Jambo la kusikitisha wanawake wawili waliwasili ukumbini saa 11 jioni na kutueleza kwamba mhusika anakuja, kweli akafika dakika ishiriki baadaye lakini akiwa mikono mitupu,” amesema.
Ngania amesema kutokana na kukiuka makubaliano aliamua kuwaita polisi na kupelekwa mahabusu, kutokana na kuwadanganya wanajamii waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kusherehekea.
Katika mahojiano na kituo cha redio cha 9 FM, Maikut amesema atawajibika kwa masuala yote yaliyojitokeza kutokana na kukiuka makubaliano.
“Nilikuwa na wenzangu ambao tuliambatana kwenye tafrija yangu, hata hivyo kuna changamoto kidogo zilikuwa zimejitokeza,” amekiri Maikut.
Kiongozi wa Kimila, Alfre Chebet amesema Maikut hakuwapa taarifa viongozi wa kimila badala yake aliendelea kufanya maandalizi kwa kushirikiana na kaka yake.
Hata hivyo, kutokana na makubaliano yaliyofanyika, Maikut amekubali kulipa faini pamoja na mahari ifikapo Desemba 30 mwaka huu.