Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajali za barabarani zaongeza vifo kwa 25% Kenya

9ded32e3d0e0dd667f56bb2ab0d49f24 Ajali za barabarani zaongeza vifo kwa 25% Kenya

Tue, 28 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IDADI ya watu waliokufa katika ajali za barabarani mwaka huu nchini Kenya imeongezeka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), umebaini kuwa, Kati ya Januari 2021 na Septemba 20, 2021, watu 3,212 wamekufa katika ajali, kukiwa na ongezeko la watu 652 kutoka vifo 2,560 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Imeelezwa sababu za ongezeko la ajali ni kuendesha ovyo, kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari, madereva kuendesha gari wakiwa wamelewa, watu kutembea barabarani wakiwa wamelewa, wapanda pikipiki kutotumia kofia ngumu na mengineyo.

Kati ya waliokufa mwaka huu, 1,111 ni watembea kwa miguu, madereva 311, abiria 520, wapanda baiskeli 61 na waendesha pikipiki 891.

Katika kipindi kama hicho mwaka jana walikufa watembea kwa miguu 927, madereva 213, abiria 331, waendesha baiskeli 63 na waendesha pikipiki 738.

Watu takribani 7,018 waliopata majeraha makubwa hadi kufikia wiki iliyopita, ni ongezeko kutoka majeraha 5,172 kwa mwaka jana huku wengine 3,938 walikuwa na majeraha madogo ikilinganishwa na 3,295 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Ajali kubwa 2,824 zimetokea mwaka huu ikilinganishwa na 2,284 zilizotokea mwaka 2020, ikiwa ni ongezeko la ajali 540 huku watembea kwa miguu 1,279 wakiwa wamepata majeraha makubwa mwaka huu, wakati mwaka jana walikuwa 984 katika kipindi kama hicho.

Kiongozi wa NTSA, George Njao, alisema watashirikiana na mashirika mengine kukabiliana na ajali za barabarani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz