Maafisa nchini Colombia wanasema watoto wanne waliotoweka tangu ndege yao kuanguka msituni wamepatikana wakiwa hai zaidi ya wiki mbili baadaye.
Mama yao na watu wazima wengine walifariki katika ajali hiyo.
Shirika la serikali la ustawi wa watoto, ICBF, limesema limepata taarifa "kutoka eneo hilo " kwamba watoto hao wamepatikana wakiwa na afya njema.
Rubani alisema pia alikuwa ameambiwa watoto hao wamepatikana na watu wa kiasili ndani ya msitu huo mkubwa.
Wanajeshi wanaoshiriki katika msako huo, hata hivyo, bado hawajawaona watoto hao wenyewe.
Ndege hiyo ndogo aina ya Cessna 206 waliyokuwa wakisafiria ilikuwa ikisafiri kutoka Araracuara, ndani kabisa ya msitu wa Amazon kusini mwa Colombia, kuelekea San José del Guaviare, ilipotoweka asubuhi ya tarehe 1 Mei.
Rubani wake alikuwa ameripoti mapema matatizo ya injini.
Baada ya msako mkubwa uliohusisha zaidi ya wanajeshi 100, hatimaye ndege hiyo ilipatikana Jumatatu, wiki mbili baada ya kutoweka.
Miili ya rubani, rubani msaidizi na Magdalena Mucutuy mwenye umri wa miaka 33, mama wa watoto hao wanne, ilipatikana katika eneo la ajali katika jimbo la Caquetá.
Lakini watoto hao ambao wana umri wa miaka 13, tisa na minne, pamoja na mtoto mchanga wa miezi 11, hawakupatikana.