Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika ijihadhari kupoteza kila kitu

31a9af55a8a10e15909fb44593a2b698.png Afrika ijihadhari kupoteza kila kitu

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ndugu msomaji wangu, wote tunakumbuka wazi kabisa moja kati ya mambo yanayolitesa Bara la Afrika ni ukoloni. Japokuwa inawezekana kuna wengine watakuwa na mtazamo tofauti kwamba labda ujio wa wakoloni uliisaidia Afrika lakini ukweli utabaki kuwa bara letu hili linaendelea kunyanyasika bado kwa sababu ya mkoloni.

Ni wazi kila penye baya kuna wanufaika na kila penye zuri kuna waumiaji vile vile. Jambo hili ndivyo lilivyo katika Bara la Afrika. Kwa muda mrefu tumeruhusu mabeberu kututawala na bahati mbaya hatujali kuona kama ni tatizo kutawaliwa hivyo.

Kuna wakati najiuliza hivi Waafrika ipo siku mawazo yetu yatabadilika? Ipo siku tutajua kwamba hakuna beberu anayeweza kutupatia msaada pasipo kutaka kitu kingine?

Katika kitabu cha “Things Fall Apart” cha Chinua Achebe kuna maneno yanayosema ‘tumeshachelewa alisema Obierika, ndugu zetu na watoto wetu wameungana na mgeni, wameungana na dini yake na wamemsaidia kusimika serikali yake. Kama tukiamua kuwaondoa wazungu katika umofia, ni rahisi sana maana wako kama wawili. Lakini je, itakuwaje kwa ndugu zetu walioungana na wazungu na wanaishi kama wao? Na wamepewa madaraka? Wanaweza kwenda umoro na walete wanajeshi, tutakuwa kama Abame.

Hivi mzungu anaelewa miiko na tamaduni zetu kuhusu ardhi? Anawezaje iwapo hawezi kuzungumza hata lugha zetu? Lakini anasema kwamba tamaduni na miiko yetu ni mbaya! Na ndugu zetu walioungana naye wanahisi tamaduni zetu ni mbaya. Unafikiri tunawezaje kupambana na hawa iwapo ndugu zetu wametenganishwa na sisi? Mzungu ni mjanja sana. Alikuja kimya kimya na dini yake, tukamkubali kwa kuona kwamba ni mjinga na hana madhara kwetu. Bahati mbaya sasa ameungana na ndugu zetu. Na sasa hatuwezi kuzungumza lugha moja. Ameweka kisu kwenye vitu vilivyokuwa vinatuunganisha na sasa tumepotezana.”

Ndugu msomaji nimependa kunukuu kipengele hiki kwasababu kinagusa maana katika makala ninayoandika leo.

Kila jambo huwa lina mwanzo. Inawezekana mwanzo usionekane mbaya lakini baadaye linapokuwa huonesha uhalisia wake na kisha lengo haswa.

Ndugu msomaji, tangu awali mkoloni anaitamani Afrika kwa kila namna. Tamanio lake ni kuona anamiliki ardhi yenye rutuba na mali asili zote zilizopo barani humo.

Bahati mbaya kama Waafrika hatujagundua hilo; kama tumegundua tunajifanya hatuoni kwa sababu kuu mbili, moja kwamba labda vile kuna anayefaidi moja kwa moja au anaandaa mazingira ya kuanza kufaidi.

Wadadisi wa mambo wanaonesha kwamba miaka ijayo Afrika ndilo bara pekee litakalokuwa na ardhi yenye rutuba na vyakula vya kutosha. Kwa Bara la Ulaya na Amerika inawezekana ardhi yao isiwe na matumizi kwa miaka ijayo. Jambo hili haliwaachi mabeberu kimya.

Kama walivyodanganya wakati wa kuja kututawala miaka hiyo kupitia dini zao na sasa wako na mbinu mbadala ya kuja kujimilikisha bara hili na kwasasa inawezekana tusiwe na uwezo wa kupambana nao kwa kuwa watakuwa wameungana kabisa pasipo kificho na ndugu zetu.

Katika kipindi cha miaka ya karibuni kumeibuka mtindo wa watu weupe (wazungu) kutaka kuoana na Waafrika sana. Bahati mbaya ndugu zetu wanawake na wanaume wamejiweka tayari kutafuta ndoa na wazungu ama kuzaa nao. Kwa sasa si ajabu kumsikia binti au kijana wa kiume akijigamba kwamba tamanio lake ni kuzaa na mzungu.

Beberu anatamani kuitawala Afrika tena pasipo kubugudhiwa na mtu yeyote. Wadadisi wa mambo wanaonesha kwamba mtindo ulipo sasa utakuwa ni kuhakikisha mtoto wa kizungu anaolewa na Muafrika kutoka kwenye familia yenye boma kubwa, kisha baada ya kuzaa naye mtoto atapewa jina la kutoka kwenye boma au familia yake.

Mtoto huyo ataenda kuishi Ulaya au Amerika lakini baada ya miaka kadhaa atarejea kudai urithi kwenye boma husika kwa kuwa ni mtoto halali tena mwenye majina halali ya kimila. Kiuhalisia mtoto huyu si Mwafrika kwa ufikiri bali kwa majina.

Kama Waafrika je, tumeliwaza hili? Je, tunajua madhara ya kuruhusu ardhi yetu kumilikiwa na mkoloni aliyepambana miaka yote atutawale? Je, uzao kama huu ukipata bahati ya kushika dola utaelewa maumivu yetu kama Waafrika? Je, utapigania maslahi ya nani?

Kama alivyosema Okonkwo katika kitabu cha Things Fall Apart, tutaweza kupambana na mkoloni iwapo tutafikia hatua hii? Iwapo tunaruhusu muingiliano huu kama Waafrika

tutaweza kujilinda na ukoloni wa namna hii? Nia yangu si kwamba watu wa mataifa, imani na rangi tofauti wasioane, ila tuangalie lililo nyuma ya ndoa hizo kama ni hili la hatari kwetu, tulikomeshe. Tuwaze kabla ya kufanya uamuzi.

Inawezekana nisieleweke katika makala haya lakini miaka mingi ijayo tutakuja kuelewa somo hili. Kwa wenzetu yaani wenye roho ya ubeberu maana si kila mzungu ni beberu, wanaweza kupanga jambo kwa muda mrefu sana. Hawaoni tatizo kufanya jambo litakalotimilika baada ya miaka 30 au 20 ijayo. Haya hufanyika ili mhusika asiweze kushtuka mpango huo.

Wazee wetu waliopigania Bara hili matamanio yao yalikuwa ni kuona Afrika inakuwa moja yenye uongozi mmoja na nguvu kubwa zaidi. Mkoloni alifanikiwa kututenganisha kwa njia alizotumia miaka hiyo.

Je, kama Waafrika tuko tayari kuruhusu kuendelea kutenganishwa pasipo kujihadhari?

Pengine, inawezekana tusione kwamba kulilinda bara letu na uzao wake wa asili ni muhimu; lakini wakati utafika ambapo uzao asilia wa Kiafrika utajikuta nusu kwa nusu na mazalia ya mkoloni ama zaidi ya nusu iwapo hatutakuwa makini katika maamuzi yetu.

Hatari nyingine ni uzao wenye hulka, tabia na uamuzi uliobeba ukoloni ndani yake, huu ni hatari zaidi hata ya uzao wa kibaiolojia. Mtu ni Mwafrika lakini ana mawazo ya kikoloni, kuangamiza wenzake kwasababu ya kitu anaponufaika nacho wakati huo.

Hii ndio sababu Afrika tunapaswa kuchukua tahadhari kwa aina zote za ukoloni, tusikubali kupoteza kila kitu maana vingi tulivipoteza wakati wa ukoloni na bado kuna wajanja wanaviwania nyakati hizi kwa njia ya ujanja ujanja.

Kama Waafrika kuna umuhimu wa kutoa elimu endelevu ya uraia kwa watu wake. Elimu hii itasaidia kulinda undugu wetu kabla ya kuruhusu undugu wa nje utakaotusumbua. Inawezekana baadhi ya viongozi wa Kiafrika wakawa wanajitahidi kulinda na kupigania maslahi yetu, lakini nguvu zao zitaharibika bure iwapo hatutashtukia mchezo huu wa kikoloni unaoendelea kwa uzao wetu.

Mungu atusaidie katika kutukumbusha wajibu wetu dhidi ya bara letu na maono ya wazee wetu.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili; +255712246001; [email protected]

Chanzo: www.habarileo.co.tz