Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameondoa kauli yake aliyoitoa Jumanne kuwa nchi hiyo itajiondoa kutoka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo imetoa hati ya kukamatwa Rais wa Russia Vladimir Putin.
Ofisi ya rais jioni Jumanne ilifuta maoni ya Ramaphosa aliyoyatoa hapo awali siku hiyo na kusema aliyatamka kimakosa aliposema chama tawala cha African National Congress (ANC) “kitajiondoa” kutoka ICC.
Matamashi yake yaliibua utata wakati Rais wa Russia Vladimir Putin, ambaye anatakiwa na ICC kwa uhalifu wa kivita nchini Ukraine, amealikwa kuhudhuria mkutano wa Agosti nchini Afrika Kusini.
Ikiwa ni nchi iliyosaini Mkataba wa Roma ambao uliunda ICC, Pretoria italazimika kumkamata Putin iwapo ataingia nchini humo.
Lakini saa chache baada ya Ramaphosa kusema kuwa chama cha ANC kitajiondoa kutoka mahakama ya The Hague, msemaji wake, Vincent Magwenya, alisema kauli yake ilikuwa na makosa.
“Afrika Kusini itaendelea kuwa ni sehemu ya mahakama ya ICC kufuatana na azimio la 55 la mkutano wa kitaifa wa ANC– uliofanyika Desemba 2022 – kubatilisha uamuzi wa awali wa kujitoa kutoka ICC,” alisema.
Magwenya alisema sahihisho hilo linafuatia kosa lililofanyika wakati wa mkutano na vyombo vya habari uliofanywa na ANC juu ya suala la Afrika Kusini na ICC, ambapo alisema rais amejutia hilo na anathibitisha “kukosea.”
Ramaphosa alisema kulikuwa na hisia ya muda mrefu ndani ya chama tawala kuwa mahakama hiyo haitendi haki kwa baadhi ya nchi.
ANC ilitaka kujiondoa kutoka ICC miaka kadhaa iliyopita lakini ilizuiliwa kufanya hivyo na uamuzi wa mahakama ya Afrika Kusini iliyogundua ni kinyume cha katiba kufanya hivyo.
Haiko bayana iwapo Putin atahudhuria mkutano huo wa kikundi cha BRICS unaozijumuisha nchi za – Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Hata kama atahudhuria, hakuna uwezekano wa kuthibitisha kuwa Afrika Kusini itamkamata rais wa Russia.
Pretoria ilikataa kutekeleza hati ya ICC ya kumkamata Rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir alipozuru Afrika Kusini 201Chama cha ANC ni rafiki mkuu wa Moscow, ambayo kama kiongozi wa Umoja wa Sovieti uliunga mkono vita vyake dhidi ya Ubaguzi wa utawala wa wazungu wachache.
Kyiv pia iliunga mkono harakati ya ANC kufikia demokrasia, lakini Pretoria hadi sasa imekataa kuilaani Kremlin kwa uvamizi wa Ukraine.