Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kusini yasitisha chanjo ya corona

B4bc95572477d4dcf7bc6d67bf397b9a Afrika Kusini yasitisha chanjo ya corona

Tue, 9 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

AFRIKA Kusini imesitisha mpango wa kutaka kuwachanja wananchi wake chanjo aina ya Oxford-AstraZeneca dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kutokana na matokeo dhaifu ya uwezo wa chanjo hiyo.

Maamuzi hayo yamefikiwa wakati wanasayansi nchini humo wakisema asilimia 90 ya maambukizi mapya ni aina mpya ya virusi vya corona. Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Zweli Mkhize, alisema serikali itahitaji ushauri wa kitaalamu wa ama kuendelea na chanjo hiyo au la baada ya kuonesha matokeo hafifu na yasiyotarajiwa.

Afrika Kusini ilipokea dozi milioni moja za chanjo ya Oxford-AstraZeneca na ilikuwa inatarajia kuanza kuwachanja watu wiki ijayo. Mkhize alisema chanjo ya Oxford-AstraZeneca haioneshi matokeo mazuri kwa wagonjwa wenye dalili za kawaida na za kadiri, hivyo serikali itatoa chanjo zilizotengenezwa na kampuni za Johnson & Johnson na Pfizer.

Alisema utafiti uliofanyika kuhusu chanjo hiyo uliowahusisha watu 2,000, na kwamba, utafiti haujaweza kuchunguza ufanisi wa chanjo katika kuzuia maambukizi makali kwa kuwa washiriki walikuwa na umri wa wastani wa miaka 31 sampuli ambayo haikisi kundi la watu wanaoweza kuwa na hatari ya kuugua zaidi wanapopatwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Hapa Tanzania Rais John Magufuli alishaweka msimamo wa kutopokea chanjo yoyote ya Covid- 19. Wakati akizindua shamba la miti Chato mkoani Geita mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kuwa waangalifu na chanjo hizo.

“Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania, lakini simameni imara. Najua wapo baadhi ya Watanzania wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine kwenda kuchanjwa, na walipochanjwa huko wametuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu, simameni imara, chanjo hazifai,”alisema.

Alisema kama chanjo za Covid-19 zingekuwa za kweli hata chanjo ya Ukimwi, kifua kikuu, malaria na saratani nazo zingekuwa zimeshapatikana, hivyo Watanzania hawana budi kuwa waangalifu na wasidhani wanapendwa sana.

Rais Magufuli alisema, si kila chanjo ni ya maana kwa taifa hivyo aliitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto isiwe inakimbilia chanjo bila kujiridhisha.

“Ni lazima Watanzania tuwe macho, ni lazima Watanzania tuwe waangalifu, tutafanyiwa majaribio ya ajabu ambayo yataleta madhara makubwa. Ninaomba tuendelee kusimama na kumuomba Mungu wetu”alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz