Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kusini yaishitaki tena Israel

Mkasa Wa Moto Johannesburg Ni 'janga Kubwa'   Rais Ramaphosa Afrika Kusini yaishitaki tena Israel

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kufuatia kuendelea jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, Afrika Kusini imeushtaki rasmi utawala huo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Haque. Mastaka muhimu ya Afrika Kusini ni jinai za kivita, mauaji ya kizazi na kikabila huko Gaza na katika maeneo mengine ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ya Palestina.

Huku ikiashiria kuwa kutokana na hatua ambazo imekuwa ikizitekeleza kufuatia mashambulizi ya tukio la 7 Oktoba, Israel imekiuka makubaliano ya 1948 ya Umoja wa Mataifa ya Kuzuia na Kutoa Adhabu dhidi ya Mauaji ya Kimbari, Afrika Kusini imetoa wito wa kuchunguzwa jinai za sasa za utawala huo.

Baada ya kuwasilisha mashtaka yake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imetangaza katika taarifa kwamba nchi hiyo ina jukumu la kuzuia mauaji ya halaiki. Huku akielezea wasiwasi mkubwa wa Afrika Kusini kuhusiana na hali mbaya ya raia wanaozingirwa katika mashambulizi yanayoendelea ya Israel katika Ukanda wa Gaza Rais wa Afrika Kusini ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki wiki ijayo kuitisha kikao kwa ajili ya kushughulikia suala hilo. Vilevile nchi hiyo imetaka kuchukuliwa hatua muhimu kwa ajili ya kusimamishwa haraka operesheni za kijeshi huko Gaza.

Hatua hiyo ya Afrika Kusini imechukuliwa huku Wazayuni wakiendeleza kwa miezi mitatu sasa mashambulizi ya kinyama ya mabomu dhidi ya raia wa kawaida huko Gaza, hasa wanawake na watoto. Kutokana na mashambulizi hayo ya mabomu, zaidi ya Wapalestina 21,700 wameuawa shahidi na zaidi ya watu elfu 54 kujeruhiwa na wengine milioni 1.5 kulazimika kuhama makazi yao katika ukanda huo. Afrika Kusini yaistaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Licha ya hatua za kinyama za Israel dhidi ya Wapalestina, lakini nchi za Magharibi hususan Marekani si tu kwamba tangu mwanzo hazijalaani vitendo hivyo vya Israel, bali zimezidisha himaya yao ya kisiasa, kijeshi na silaha kwa Tel Aviv. Hii ni katika hali ambayo tokea hapo awali jumuia za kimataifa na mashirika huru ya kiraia na kibinadamu ulimwenguni kote pamoja na kulaani jinai za Israel yametaka kukomeshwa mara moja vita na mauaji dhidi ya Wapalestina wasiokuwa na hatia yoyote.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi za Kiafrika ambazo tokea yalipoanza mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya Wapalestina zimetoa radiamali na kulaani hatua hizo za kinyama za Wazayuni dhidi ya wananchi wasiokuwa na ulinzi wa Gaza. Aghalabu ya nchi hizo ambazo zilitawaliwa kwa miaka mingi na nchi za Magharibi na kukumbana na ukoloni, unyonyaji na ubaguzi wa rangi sambamba na kulaani jinai za Israel, zimetaka kukomeshwa ukatili unaofanyiwa wananchi wanaozingirwa wa Gaza. Afrika Kusini, ikiwa ni nchi ambayo ilikumbana na mateso ya utawala wa kibaguzi kwa miongo kadhaa na inayoongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani, ilianzisha juhudi za kukomesha mauaji ya Wapalestina tangu mwanzoni mwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza kufuatia Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba na sasa, imefikisha malalamiko yake mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel ikiwa ni katika kuendeleza juhudi zake hizo katika uwanja huo. Kuhusiana na hilo, Naldi Mandisa Pandour, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema: 'Ulimwengu lazima uilazimishe Israel kusitisha jinai zake dhidi ya binadamu huko Gaza.' Kuendelea jinai za wazayuni huko Gaza

Kwa hakika, uzoefu wa machungu ya kihistoria ya Afrika Kusini yaliyosababishwa na siasa za ubaguzi wa rangi umewapelekea viongozi wa nchi hiyo kutangaza kwamba hawataruhusu kuwepo serikali nyingine ya ubaguzi wa rangi duniani.

Naldi Pandor amesema katika muktadha huo: 'Afrika Kusini inaamini kwamba Israel inapaswa kutajwa kuwa serikali ya ubaguzi wa rangi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapaswa kuunda kamati kuhusu jambo hilo.'

Kwa sasa ni zamu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kama chombo cha mahakama cha Umoja wa Mataifa, kushughulikia kesi ya wazi kabisa ya mauaji ya kimbari katika miongo michache iliyopita na kuitaka jumuiya ya kimataifa ikomesha jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina, hasa wa Ukanda wa Gaza. Vinginevyo, itibari na uhalali wa taasisi kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki utapotea machoni mwa nchi nyingi za ulimwengu na fikra za waliowengi duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live