Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuhusu kufukuzwa ujumbe wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika uliofanyika Addis Ababa huko Ethiopia kuwa utawala wa Kizayuni umetenda jinai nyingi dhidi ya Palestina na suala hilo ni kinyume na hati ya Umoja wa Afrika.
Mkutano wa 36 wa wakuu wa Umoja wa Afrika (AU) ulifanyika wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Hata hivyo kabla ya kuanza rasmi mkutano huo askari usalama waliufukuza ukumbuni ujumbe wa utawala wa Kizayuni wa Israel; kitendo kilichoungwa mkono na makundi ya Palestina na kuwakasirisha Wazayuni.
Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ametangaza kuwa ujumbe wa utawala wa Kizayuni ulifukuzwa katika mkutano huo wa Addis Ababa kutokana na kuendelea kutenda jinai na uhalifu dhidi ya wananchi wa Palestina na upinzani wa nchi za Afrika dhidi ya suala la kupatiwa utawala wa Kizayuni hadhi ya kuwa mwanachama mtazamaji ndani ya Umoja wa Afrika.
Naledi Pandor ameongeza kuwa, Afrika Kusini inapinga suala la utawala wa Kizayuni kupewa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika kwa sababu utawala huo unaendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kujenga vitongoji vipya vya walowezi, na hauheshimu thamani, kanuni na malengo ya Hati ya Umoja wa Afrika.
Matamshi haya ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini yamekaribishwa na kupongezwa na makundi ya Wapalestina na wanaharakati wa kupigania uhuru kote duniani.
Katika lugha kali isiyo ya kawaida, taarifa ya mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa ililaani "mienendo ya kikoloni ya Israel katika maeneo ya Palestina inayoyakalia kwa mabavu, kuwabagua Wapalestina kwa misingi ya rangi na dini, na kuwapa Waisraeli haki na upendeleo zaidi juu ya Wapalestina ambao ni wamiliki wa ardhi wa Palestina."
Wakuu wa nchi za Kiafrika pia waliunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa na kutoa wito wa kuungwa mkono kimataifa suala hilo.