Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kusini yaikalia kooni ICJ kuhusu Israel

ICJ Dhidi Ya Israel Afrika Kusini yaikalia kooni ICJ kuhusu Israel

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Afrika Kusini imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) itoe ushauri wa kisheria unaosema kuwa hatua ya Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.

Mawakili na wataalamu wa sheria wa Afrika Kusini wameiambia ICJ leo Jumanne kuwa, Israel imekanyaga sheria za kimataifa kwa kuendelea kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina, sanjari na na kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

Vusimuzi Madonsela, Balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi amewaambia majaji ya ICJ kuwa, suluhu ya 'kuundwa mataifa mawili' kutatua mgogoro wa Israel na Palestina haitoshi tena, na kwamba ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina unapaswa kutangaza kuwa haramu.

Jumatatu ya jana, Mahakama ya ICJ ilianza kusikiliza shauri la kuamua kuhusu uhalali wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kuzivamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Shauri hilo liliwasilishwa mahakamani hapo kufuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) la mwishoni mwa mwaka 2022. Nchi zaidi ya 50 zitawasilisha hoja zao katika mahakama ya ICJ hadi Februari 26. Mahakama ya ICJ

Wanasheria na wawakilishi wa Palestina jana walizungumza mbele ya ICJ na kusisitiza kwamba, uvamizi wa Israel ni kinyume cha sheria kwa sababu umekiuka kanuni muhimu za sheria za kimataifa.

Utawala wa Kizayuni haujatuma mwakilishi wake kwenye kikao hicho cha ICJ, lakini umetuma taarifa ukidai kuwa maoni ya kisheria yatakatolewa na mahakama hiyo ya mjini The Hague yatakuwa na taathira hasi kwa juhudi za kufikia mapatano na Wapalestina.

Majaji wa ICJ wanatazamiwa kutumia takriban miezi sita kupitia hoja zitakazowasilishwa, kabla ya kutoa ushauri wake wa kisheria juu ya shauri hilo, ambalo pia limeitaka korti hiyo ya kimataifa kugusia juu ya taathira hasi za kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live