Mamlaka husika za Afrika Kusini zimesema kuwa zimefanya msako na mashambulizi ya kushtukiza katika majimbo matano nchini humo jana Alhamisi ili kusambaratisha genge la magendo ya makaa ya mawe linalolaumiwa kuiba zaidi ya dola milioni 26 za mauzo ya makaa ya mawe.
Mamlaka ya Ushuru na Mapato ya Afrika Afrika Kusini imeeleza kuwa, genge moja la uhalifu liliyaamuru malori yenye makaa ya mawe kuelekea katika vituo vya kuzalisha umeme na kisha likaiba makaa hayo ya mawe kwa ajili ya kuyauza. Walibadilisha makaa ya mawe yaliyokuwa kwenye malori mkabala wa bidhaa nyingine duni.
Mamlaka ya Ushuru na Mapato ya Afrika Kusini imeshirikiana na wakala wengine wa usalama kuendesha msako na oparesheni kushtukiza katika majimbo ya Gauteng, Mpumalanga, KwaZulu-Natal, Free State na Limpopo. Hata hivyo hadi sasa hakuna mtu au kundi lililotiwa mbaroni kwa wizi wa makaa ya mawe. Wizi wa makaa ya mawe Afrika Kusini
Afrika Kusini nchi yenye uchumi mzuri zaidi barani Afrika inakabiliwa na tatizo la umeme linalosababishwa na kutokana na kushindwa kwa vituo vyake kuzalisha umeme unaohitajika kwa ajili ya watu milioni 62 wa nchi hiyo. Shirika la umeme linalomilikiwa na serikali, Eskom, linazalisha karibu asilimia 95 ya nishati ya umeme huko Afrika Kusini.
Kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini Afrika Kusini kunatajwa kusababishwa na ufisadi na uongozi mbovu wa miaka kadhaa sasa ndani ya Shirika la Eskom huku washukiwa wanaodaiwa kujihusisha na magendo ya makaa ya mawe wakitajwa kuwa ni pamoja na wafanyakazi kadhaa wa zamani wa shirika hilo.