Afrika Kusini imesema itahalalisha biashara ya ngono kupitia mapendekezo ya marekebisho yatakayoshinikizwa na waziri wa sheria.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Jinai (Makosa ya Kujamiiana na Mambo Yanayohusiana) uliidhinishwa na baraza la mawaziri mwishoni mwa mwezi uliopita.
Inatafuta kuhalalisha uuzaji na ununuzi wa huduma za ngono za watu wazima, wizara ilisema.
Ilichapishwa Ijumaa kwa maoni ya umma na italazimika kupitishwa na bunge. "Inatarajiwa kuwa kuhalalisha kutapunguza ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wafanyabiashara wa ngono," Waziri wa Sheria Ronald Lamola alisema.
Aliongeza: "Pia itamaanisha upatikanaji bora wa huduma za afya na huduma za afya ya uzazi kwa wafanyabiashara ya ngono." Shirika la habari la AFP linanukuu kundi la kutetea haki za wafanyabiashara ya ngono la SWEAT likisema:
"Kwa kuwa wafanyabiashara ya ngono hawatajwi tena kama wahalifu, wanaweza kufanya kazi vizuri zaidi na polisi ili kukabiliana na vurugu".
SWEAT ilikaribisha mswada huo kama "habari za kushangaza".
Sheria zinazokataza watoto kuhusishwa na biashara ya ngono na usafirishaji haramu wa binadamu kwa madhumuni ya ngono zitaendelea kutumika.