Jeshi la Afrika Kusini limetangaza kuwa mwezi ujao litafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Urusi na China katika maeneo ya pwani yake.
Mazoezi hayo yatafanyika kwa siku 10 kuanzia tarehe 17 Februari hadi 27 Februari katika mji wa bandari wa Durban na Richards Bay.
Lengo ni kubadilishana ujuzi na maarifa ya kiutendaji, Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini (SANDF) lilisema.
Afrika Kusini ilikuwa miongoni mwa nchi za Kiafrika ambazo zilijiepusha na kuunga mkono uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Nchi hiyo ilichukua uenyekiti wa kundi la mataifa ya Brics - ambalo linajumuisha Brazil, Urusi, India na China - mwezi uliopita.
Hii itakuwa mara ya pili kwa mazoezi hayo ya kijeshi kufanyika.
Ya kwanza ilifanyika mnamo Novemba 2019 huko Cape Town.
"Zoezi la mwaka huu litashuhudia zaidi ya wafanyakazi 350 wa SANDF kutoka idara mbalimbali za huduma na washiriki," ilisema SANDF.