Afrika Kusini imesema itaendelea kustafidi na teknolojia ya shirika la China la Huawei licha ya kushinikizwa na Marekani iachane na kampuni hiyo.
Anil Sooklal, Balozi wa Pretoria barani Asia na katika kundi la BRICS amesema hayo kwenye hotuba yake katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal na kueleza kuwa, "Kuna mashinikizo makubwa kutoka serikali ya Washington inayotutaka tuache kutumia teknolojia ya Huawei."
Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Afrika Kusini amesema serikali ya Pretoria haitasalimu amri na kukatiza ushirikiano wake na Huawei ya China, licha ya mashinikizo hayo ya Washington.
Balozi huyo wa Afrika Kusini amekumbusha kuwa, teknolojia ya shirika la mawasiliano la Huawei la China imepigwa marufuku nchini Marekani na katika ghalabu ya nchi za Ulaya.
Huawei imekuwa ikizipa ushindani kampuni za mawasiliano za US kama Apple Ikumbukwe kuwa, mwaka 2019, serikali ya Marekani ililiwekea vikwazo shirika hilo kubwa la kiteknolojia la China Huawei na hivyo kupelekea uhusiano wake na China ambao umezorota kuwa mbaya zaidi.
Marekani na kwa visingizio tofauti vikiwemo vitisho vya kiusalama, imekuwa ikishadidisha mashinikizo dhidi ya washirika wake likiwemo Shirika la Huawei ambalo ni shirika kubwa la mawasiliano la China, kuuza bidhaa zake ndani ya taifa hilo.
Maafisa wa Marekani wamekuwa wakidai kuwa, shirika hilo la mawasiliano la Huawei linaisaidia serikali ya Beijing kufanya ujasusi.