Afisa mmoja mashariki mwa Libya amekanusha madai kuwa wengi wa waliopoteza maisha katika mafuriko yaliyotokea wikendi iliyopita waliambiwa wakae majumbani mwao.
Othman Abdul Jalil, msemaji wa serikali yenye makao yake mjini Benghazi, aliambia BBC kwamba wanajeshi walionya watu katika mji wa Derna na kuwataka kuondoka.
Alikanusha madai kuwa watu waliambiwa wasihame, lakini alikubali kuwa huenda wengine walihisi tishio hilo lilitiwa chumvi.
Wakati huo huo, timu za BBC mjini Derna zinasema mashirika ya misaada bado hayajafika katika jiji hilo.
Wakati waandishi wa habari wakishuhudia msururu wa shughuli katikati ya Derna - waokoaji, wafanyakazi wa ambulensi na timu za uchunguzi zikifanya kazi kubaini waliofariki - kulikuwa na dalili ndogo ya mashirika makubwa ya misaada ya kimataifa.
Msemaji wa shirika moja alisema kuwa kujaribu kuratibu shughuli za usaidizi nchini humo ni "ndoto".
" Wiki moja iliyopita, Libya ilikuwa tayari kwenye hali ngumu," alisema Tomasso Della Longa kutoka Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Red Crescent Societies (IFRC).
Kufanya hali kuwa ngumu zaidi ni ukweli kwamba mafuriko yameharibu miundombinu muhimu, kama vile barabara na mifumo ya mawasiliano ya simu.
Idadi ya vifo ambayo imetolewa inatofautiana kutoka karibu 6,000 hadi 11,000. Huku maelfu zaidi wakiwa bado hawajulikani walipo, meya wa Derna ameonya kwamba jumla inaweza kufikia 20,000.
BBC imeambiwa kuwa baadhi ya miili ya waathiriwa imesongea ufukweni zaidi ya kilomita 100 (maili 60) kutoka Derna, baada ya kusombwa na maji hadi baharini.
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu, Jens Laerke, aliambia BBC kwamba bado kuna manusura na maiti chini ya vifusi, na kwamba itachukua muda kabla ya kujua idadi halisi ya waliopoteza maisha.
"Tunajaribu kusiwe na janga la pili huko. Ni muhimu kuzuia shida ya kiafya, kutoa makazi, maji safi na chakula," alisema.
Zaidi ya watu 1,000 hadi sasa wamezikwa katika makaburi ya halaiki, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limewataka wafanyakazi wa majanga kuacha kufanya hivyo, kwa sababu kuzikwa kwa haraka kwenye makaburi ya halaiki kunaweza kusababisha msongo wa mawazo wa muda mrefu kwa wanafamilia wanaoomboleza.
Maelfu ya watu waliuawa wakati mabwawa mawili ya maji yalipopasuka baada ya kimbunga Daniel kukumba eneo hilo siku ya Jumapili, na kusomba vitongoji vyote kwenye Bahari ya Mediterania.
Walionusurika wameelezea kunusurika kwa namna ya kutisha na watu kusombwa mbele ya macho yao.