Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki Siku 10 tu Baada ya Kuwasili Saudi Arabia Kufanya Kazi za Ndani

Wanja Afariki Siku 10 tu Baada ya Kuwasili Saudi Arabia Kufanya Kazi za Ndani

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

FAMILIA moja Mjini Mombasa nchini Kenya inaomboleza kifo cha binti yao kilichotokea siku 10 tu baada ya kutua nchini Saudi Arabia kufanya kazi ya usafi. Lucy Wanja mwenye umri wa miaka 35 alifunga safari ya kuelekea Uarabuni, Septemba 12, 2021 kwa lengo la kutengeneza kipato baada ya nafasi hiyo kutoipata kwa miaka mingi.

Imearifiwa kuwa siku 10 baada ya kuwasili katika eneo ambalo lilikisiwa kuwa ukurasa mpya na wenye fanaka katika maisha yake, familia ya Wanja ilijulishwa kuwa binti yao alikuwa katika hali mahututi baada ya kuanguka bafuni akioga, lakini baadaye walianza kupokea ripoti kinzani kuhusu kifo hicho jambo ambalo liliibua maswali mazito.

Awali walielezwa kwamba amefariki kutokana na mshtuko wa moyo na baadaye kuambiwa kuwa alifariki kutokana na virusi vya Corona.

Mwili wake uliwasili nchini siku chache zilizopita huku hisia zikimzidi mamake Susan Nzilani ambaye alishindwa kuamini uhalisia wa kuwa mwanawe ameaga dunia katika mazingira ambayo familia haikuyaelewa.

“Wameleta maiti badala ya kuleta mwanangu mpendwa. Mwanangu alikuwa katika hali nzuri ya afya na sijui kilichotokea alipowasili kule,” alisema mama huyo akitokwa na machozi. Familia inapanga kuufanyia upasuaji mwili wa mtoto wao ili kubaini chanzo cha kifo hicho, huku vilevile ikizitaka Serikali za Kenya na Saudi Arabia kuingilia kati.

Mwaka 2018, Wanja alijaribu kusaka nafasi ya ajira jijini Dubai lakini akatapeliwa shilingi 105,000 na shirika moja la ajira. Katika taarifa tofauti ripoti ya serikali ilifichua kuwa Wakenya 89 walikuwa wamefariki nchini Saudi Arabia katika muda wa miaka miwili iliyopita huku katibu wa vyama vya wafanyakazi Francis Atwoli akidai kuwa 'majeneza huletwa katika uwanja wa ndege wa JKIA kila asubuhi.'

Chanzo: www.tanzaniaweb.live