Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AfDB yaidhinisha ruzuku ya dola milioni 7 nishati jadidifu

3903beaac076d8fb1200c59637e119d2 AfDB yaidhinisha ruzuku ya dola milioni 7 nishati jadidifu

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) imeidhinisha ruzuku ya Dola milioni saba kutoka Mfuko wa Nishati Endelevu kwa Afrika (SEFA) kwa ajili ya msaada wa kiufundi katika kuanzisha mpango wa kuongeza kasi ya gridi ya nishati mbadala barani Afrika.

Programu ya kuongeza kasi ya soko la gridi ndogo Afrika (AMAP) ambayo inakusudia kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala katika maeneo ya mbali na kuimairisha utulivu wa hali ya hewa kote Afrika, itajumuisha mambo matatu ambayo ni utekelezaji wa mfumo mpya na usanifu wa kiwango cha kitaifa cha kuongeza kasi kwa gridi ndogo (MAPs) .

Mambo mengine ni usanifu na uboreshaji wa upatikanaji wa kifedha, msaada wa maarifa, uvumbuzi na shughuli za ukuzaji ujuzi pamoja na mwendelezo wa tovuti ya dawati la msaada la benki hiyo.

“Gridi ndogo ni sehemu muhimu ya suluhisho la upatikanaji wa nishati, siyo tu kwa maana ya kuleta mwanga katika kaya, lakini pia katika kuhakikisha watu wasio na huduma hiyo, wanapata nishati hiyo kwa matumizi yenye tija ili kuwezesha ukuaji wa uchumi jumuishi; AMAP inasisitiza AfDB kuimarisha tasnia ya gridi ndogo za Afrika ambazo ni muhimu kwa kasi ya upatikanaji wa nishati na uthabiti wa hali ya hewa,” alisema Makamu wa Rais wa benki hiyo Dk Kevin Kariuki anayehusika na nishati na hali ya hewa.

Alisema kwa kutumia uzoefu wa miaka mingi katika kujenga tasnia ya gridi ndogo Afrika, lengo la AMAP ni kubadilisha kiwango cha uwekezaji wa umma na wa kibinafsi katika gridi ndogo za nishati jadidifu kote Afrika pamoja na mipango kama vile Programu ya Maendeleo ya Soko la gridi ndogo, Mradi wa Kitaifa wa Umeme Nigeria na Programu ya gridi ya kijani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa AfDB, awamu ya awali ya ruzuku hiyo itaenda katika nchi nne na inatarajiwa kuwa na uunganishaji mpya wa umeme kwa watu zaidi ya milioni nne, kutoa Megawati zaidi ya 80 za nishati jadidifu, kutengeneza ajira za kudumu 7,200 ambapo ajira 1,800 kati ya hizo zinatarajiwa kuwanufaisha wanawake, kupunguza tani zaidi ya milioni 6.5 za hewa ya ukaa katika uzalishaji wa hewa chafu, pamoja na uwezeshaji wa wastani wa Dola milioni 650 kwa uwekezaji wa umma na binafsi katika gridi ndogo.

AfDB ilisema kuwa AMAP imeunganishwa katika matarajio ya mpango mpya wa nishati wa benki hiyo kwa Afrika pamoja na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waendelezaji wa Gridi Ndogo Afrika (AMDA), Aaron Leopold alisema :“Gridi ndogo ni jambo la msingi lakini lisiloungwa kwa mustakabali wa nishati barani Afrika; ili kufikia lengo namba saba (SDG7) la Mpango wa Maendeleo Endelevu linalolenga nishati, sekta hiyo lazima ipewe nguvu, na ili kufanya hivyo, mpango kamili wa msaada unaoainishwa na mahitaji ya tasnia unahitaji kuzileta serikali, wawekezaji na sekta ya gridi ndogo pamoja ili kurahisisha maendeleo ya haraka na madhubuti.”

Chanzo: habarileo.co.tz