Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia umetangaza kuanza uchunguzi kuhusu sababu za ajali ya helikopta ya kikosi cha kulinda amani cha umoja huo iliyotokea nchini Somalia.
Mohammed El-Amine Souef, mjumbei maalumu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali hiyo ya helikopta na kuwatakia majeruhi ahueni ya haraka.
El-Amine Souef amesema Umoja wa Afrika umenza kuchunguza sababu na chanzo cha ajali hiyo.
Watu watatu wamefariki na wengine wanane kujeruhiwa wakati helikopta ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia ilipoanguka Jumamosi katika eneo la Lower Shabelle nchini humo.
Taarifa ya Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) imesema abiria 11, wakiwemo maafisa wa jeshi la Somalia, walikuwa ndani ya helikopta hiyo. Helikopta hiyo ilikuwa kwenye operesheni ya pamoja ya kuelimishana kwa ajili ya mazoezi ya uokoaji majeruhi (CASEVAC).
Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kinaisaidia serikali kuu ya Somalia katika vita vyake dhidi ya magaidi wakufurishaji wa al Shabaab.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.