KOCHA Mkuu wa AS Kigali, Eric Nshimiyimana amewataka wachezaji wake kujiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambao utaanza baadae mwezi huu wakilenga kucheza hatua ya makundi.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza Novemba 20-22, lakini ratiba kamili haijapangwa na haijajulikana lini na jinsi gani timu zitakutana.
Timu hiyo inayodhaminiwa na Jiji la Kigali imekuwa katika mazoezi makali tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita na tayari imeshacheza mechi mbili za majaribio dhidi ya APR. Mechi zote mbili zilimalizika kwa sare ya 1-1.
AS Kigali ambayo inafundishwa na Nshimiyimana ilipata nafasi hiyo ya kucheza mashindano hayo ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya mashindano ya Kombe la Amani kuahirishwa mwaka huu kutokana na janga la virusi vya corona. Timu hiyo ndio mabingwa wa msimu wa mwaka 2019.
“Kwa kweli lengo letu ni kufikia hatua ya makundi…Tuna timu nzuri, na wachezaji wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii. Tuna matumaini hatutakuwa na majeruhi wakati wote wa kampeni," alisema mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Rwanda.
AS Kigali ilitolewa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika msimu wa mwaka 2018/19 katika raundi ya kwanza, mbele ya timu ya Uganda ya Proline, baada ya kuitoa timu ya Tanzania ya KMC katika raundi ya awali.
Klabu hiyo ina matumaini makubwa ya kufanya vizuri baada ya kurudi kwa Pierrot Kwizera aliyetumia karibu msimu uliopita akiwa nje ya uwanja kutokana na maumivu. Kiungo huyo wa Burundi alianza mazoezi na wenzake wiki iliyopita.
Baada ya kusaini baadhi ya majina makubwa katika soka la nyumbani kama beki
Emery Bayisenge na washambuliaji Muhadjiri Hakizimana na Abeddy Biramahire, AS Kigali itakuwa ikiangalia kupambana ili kutwaa taji laLigi Kuu ya Rwanda msimu ujao.
Ligi Kuu ya Rwanda inatarajia kuanza Desemba 4.