Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ANC, yazindua kampeni yake ya uchaguzi

ANC Kampeni Ramaphosa.png ANC, yazindua kampeni yake ya uchaguzi

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ANC imezindua kampeni zake za uchaguzi siku ya Jumamosi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Mei 29 nchini Afrika Kusini. Kutokana na kuongezeka kwa kutoridhika katika hali mbaya ya kijamii na kiuchumi, chama hicho cha kihistoria kinaweza kupoteza idadi kamili ya wabunge kwa mara ya kwanza.

Kikiwa madarakani tangu ujio wa demokrasia nchini humo na ushindi wa Nelson Mandela mwaka 1994, Chama cha African National Congress cha Rais Cyril Ramaphosa, kinachokabiliwa na kashfa za ufisadi, kinaona ushujaa wake ukizidi kupigwa vita, katika muktadha wa ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa unaozidi kuongezeka.

Hata hivyo chama hicho, kinasalia kuwa chombo cha kutisha cha uchaguzi na bado kinaweza kutegemea uungwaji mkono wa Waafrika Kusini wengi ambao wanakumbuka kwa fahari jukumu lake muhimu katika vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

"Katika muda wa miezi mitatu ijayo, tutawaeleza mamilioni ya raia wenzetu kwa nini ANC inasalia kuwa chama bora zaidi kwa uchaguzi wa 2024," Bw. Ramaphosa, 71, amewaambia makumi ya maelfu ya wafuasi waliokusanyika katika uwanja wa michezo nje kidogo ya jiji la Durban, mji mkuu wa KwaZulu-Natal (KZN, mashariki).

"Ndani ya miaka 50, urithi wa ukoloni wa ubaguzi wa rangi na mfumo dume, ambao bado umeenea nchini Afrika Kusini, utakuwa wa historia ya kale," amebainisha.

Mkuu huyo wa nchi pia ameahidi kuwa wagombea wa ANC katika uchaguzi wa mwezi Mei watachunguzwa kwa makini uadilifu wao.

Makumi ya maelfu ya watu waliovalia rangi za njano na kijani za chama wamehudhuria mkutano huu wa kwanza wa kampeni ya ANC katika uwanja wa mpira wa miguu wa Durban.

"Tulizaliwa na chama hiki cha kisiasa na tutaendelea nacho katika hali zote," Sthabile Nxumalo, 30, meneja wa duka la vipodozi ameliambia shirika la habari la AFP. - Serikali ya muungano? -

Zaidi ya wapiga kura milioni 27 waliojiandikisha, kati ya wakazi milioni 62, wameitwa kupiga kura Mei 29 ili kuwachagua wabunge wao ambao watamchagua rais ajaye.

Kulingana na kura za maoni, ANC inaweza kupoteza wingi wake kamili katika Bunge la taifa na kulazimishwa kuunda serikali ya mseto.

Jimbo la KwaZulu-Natal, ambalo lina watu wengi zaidi nchini, ni ngome ya kihistoria ya ANC. Lakini chama cha kwanza cha upinzani, Democratic Alliance (DA), kinaingia katika jimbo hilo na rais wa zamani Jacob Zuma (2009-2018), ambaye alijiunga na chama kipya, bado ana msingi wenye nguvu katika eneo hili alikozaliwa.

Aliyekuwa nguzo ya ANC, rais wa zamani mwenye chuki na mvuto mwenye umri wa miaka 81 alitangaza mwezi Desemba kwamba alikuwa akifanyia kampeni chama kidogo chenye itikadi kali kiitwacho Umkhonto We Sizwe (MK), kilichoundwa hivi karibuni. Chama cha ANC kilitangaza kukifuta mara moja.

Wafuasi wa ANC walimlenga rais huyo wa zamani siku ya Jumamosi, wakipeleka jeneza ndani ya uwanja lililokusudiwa kuwakilisha kifo cha mapema cha chama chake kipya.

"Zuma anawakilisha tishio kubwa zaidi kwa ANC katika KwaZulu-Natal," kulingana na Zakhele Ndlovu, profesa wa siasa katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal.

Katika ngazi ya kitaifa, chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance, ambacho bado kinatambulika kama chama cha wazungu, kilianzisha muungano na vikundi kumi vidogo vya kisiasa kushinda ANC.

Mvutano huo unafuatiliwa kwa karibu katika kura za maoni na chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema. - Uhalifu na ukosefu wa ajira unaongezeka -

Vyama viwili vya upinzani ambavyo tayari vimeanzisha kampeni zao, vinaegemea kwenye ahadi za kutengeneza ajira, kupunguza baadhi ya viwango vya uhalifu vilivyokithiri duniani na kumaliza tatizo kubwa la umeme ambalo linazorotesha uchumi wa nchi inayoongoza kwa viwanda barani Afrika.

Afrika Kusini pia ilirekodi karibu mauaji 84 kwa siku kati ya mwezi wa Oktoba na Desemba, kulingana na takwimu za hivi punde za polisi. Na miezi mitatu kabla ya uchaguzi, kiwango cha ukosefu wa ajira kimepanda tena hadi 32.1%.

"Changamoto kubwa kwa ANC itakuwa, licha ya matatizo mengine yote na kushuka kwake yenyewe, kujionyesha kama chama kikubwa, chenye nguvu ambacho kinaweza kubadilisha mambo kweli," amesema Susan Booysen wa Taasisi ya Mapungubwe ya Fikra za Kimkakati.

"Kabla ya mwaka 1994, hatukuwa na kitu. Sasa tuna elimu ya bure, nyumba, kumekuwa na maendeleo mengi," anaelezea Nomawethu Dlangisa, mwalimu mwenye umri wa miaka 52 ambaye alikuja kuhudhuria mkutano wa Durban.

Lakini hafichi huruma yake kwa Jacob Zuma, akitoa mfano wa changamoto iliyotolewa na rais wa zamani kwa ANC katika eneo muhimu la KwaZulu-Natal: "Nampenda Ramaphosa lakini pia nampendelea Zuma."

Kwa sasa ANC ina viti 230 kati ya 400 (57.50%) katika Bunge la taifa huku DA na EFF wakiwa na viti 84 na 44 mtawalia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live