Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya Huawei inanyemelea kulidaka soko la Ulaya katika bidhaa yake ya 5G ambayo ni mpya katika ulimwengu wa huduma za mtandao wa internet.
Mwishoni mwa mwezi uliopita kampuni hiyo ya Kichina ilifanya uzinduzi wa huduma na bidhaa zake jiji London, Uingereza huku vigogo wake wakisema 5G inaleta thamani mpya.
Huduma ya 5G ambayo kwa mara ya kwanza imevumbuliwa na Huawei inapingwa vikali nchini Marekani kwa kile kinachoelezwa kuwa inaweza kutumiwa kwa shughuli za kijasusi za China lakini Huawei imetangaza mpango wake wa kujenga kiwanda cha mtandao huo nchini Ufaransa kwa ajili ya soko la Ulaya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi nchini Uingereza Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Huawei Carrier’s BG alisema lengo la mpango huo ni kufanikisha ujenzi mfumo wa 5G na kufanikisa biashara yake.
“Mpaka sasa Huawei imepata zabuni 91 za kuunganisha mtandao wa 5G, Tumedhamiria kutoa huduma iliyo bora tukiwa ndiyo wa kwanza kutoa huduma hiyo, Katika zama za 4 G watu wamefurahia kubadilishana taarifa na kwa uwepo wa 5G watu watafurahia zaidi kuliko awali”.
Amesema uzoefu huo mzuri wa mawazo na hisia utaleta thamani mpya katika maisha na kimsingi 5G itabadilisha mengi na Huawei kwa kipindi cha miaka mitano ijayo inatarajia kutumia Dola za Kimarekani milioni 20 (takribani Sh50 bilioni) ili kufanya ubunifu zaidi katika mtandao huo.
Pia Soma
- Jinsi Misri inavyorudi Afrika kwa kasi
- Lema ashikiliwa na polisi mkoani Singida
- Ujenzi wa daraja lililokatika Moro-Dodoma waanza