Viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametangaza kuuliwa watu 20 katika shambulio lililofanywa na magaidi wa kundi la Daesh (ISIS) nchini humo.
Kundi la Daesh limedai kuwa limehusika katika shambulio dhidi ya kijiji kimoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuuwa watu 20. Kundi hilo limedai kuhusika na mauaji hayo kupitia taarifa iliyotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram.
Hujuma hiyo ya kigaidi iliyotekelezwa Ijumaa iliyopita huko Musandaba, kijiji kinachopatikana nje kidogo ya mji wa Beni, ni sehemu ya wimbi la uhalifu na ukatili unaofanywa dhidi ya raia; ambapo jeshi la Kongo na serikali za mitaa zinalitupia lawama kundi la waasi wa Allied Democratic Forces kundi la wapiganaji wenye silaha la Uganda lenye makao yake mashariki mwa Kongo kuwa linahusika katika kuchochea machafuko mashariki mwa Kongo.
Itakumbukwa kuwa kundi la waasi wa ADF lilitangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
Kanali Charles Omeonga, afisa wa jeshi wa eneo la Beni amesema kuwa juzi Ijumaa walihesabu jumla ya watu 20 waliouawa katika hujuma ya uvamizi kijijini huko Musandaba. Anthony Mwalushay, Msemaji wa Jeshi katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini ambako kumejiri shambulio hilo ameeleza kuwa wavamizi walitumia mapanga kukabiliana na jeshi.
Huku haya yakiripotiwa, wiki hii kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimelaani mauaji mengi ya umati yaliyofanywa na kundi la waasi wa ADF katika jimbo jirani la Ituri ambapo watu 30 waliuawa.