Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

15 wauawa kwenye maadamano kupinga askari wa UN

UN MAANDAMANO DRC Watano wauawa kwenye maadamano kupinga askari wa UN

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takriban watu watano wameuawa na wengine hamsini kujeruhiwa Jumanne katika siku ya pili ya maandamano ya kupinga uwepo wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na serikali.

Waandishi habari katika eneo la tukio walisema walinda amani wa Umoja wa Mataifa walifyatua gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kwa umati wa watu waliokuwa wanaandamana kwa amani, na kuua watu kadhaa na kujeruhi wengine wengi. Maafisa wa jeshi na polisi waliotumwa kwenye eneo la tukio hawakufyatua risasi. Mwanajeshi na polisi waliokuwa wamevalia fulana ya kuzuia risasi pia walipigwa risasi.

Mwandishi wa habari wa AFP pia aliripoti kuona mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa akimpiga risasi muandamanaji.

Maandamano ya kupinga kile kinachoonekana kutofanya kazi kwa operesheni ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO dhidi ya makundi yenye silaha nchini humo, yalianza Jumatatu.

Mamia ya watu walifunga barabara na kuimba nyimbo za kupinga Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu kabla ya kuingia katika makao makuu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani huko Goma, kitovu muhimu cha kibiashara cha jimbo la Kivu Kaskazini.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, unaojulikana kama MONUSCO, umekuwa ukikosolewa mara kwa mara na wenyeji kutokana na kutoweza kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanazunguka katika eneo hilo lenye hali tete, ambapo mauaji ya raia ni jambo la kawaida na mizozo imesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.

Maandamano hayo yanakuja baada ya rais wa Seneti ya DRC, Modeste Bahati, kuwaambia wafuasi wake mjini Goma mnamo Julai 15 kwamba MONUSCO inapaswa "kufunga virago".

Umoja wa Mataifa ulipeleka askari wake kwa mara ya kwanza mashariki mwa DRC mwaka 1999. Kikosi hicho kilipewa jina la MONUSCO – yaani Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - mwaka 2010, ukiwa na mamlaka ya kutekeleza oparesheni za kishambulizi.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, MONUSCO kwa sasa ina askari wapatao 16,300 na kumekuwa na vifo 230 kati yao. Hatahivyo kikosi hicho kimeshindwa kukabilina na waasi na sasa wananchi wanataka kiondokeo katika nchi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live