Jumla ya watu 12 wamepoteza maisha baada ya Basi la Mkombe Luxury lililokuwa linatoka nchini Afrika Kusini kuja Tanzania kugongana uso kwa uso na Lori la Mizigo eneo la Sereje nchini Zambia.
Katika idadi hiyo abiria saba kati ya 37 waliokuwa wamepanda kwenye basi hilo walipoteza maisha hapo hapo ikiwemo madereva wawili wa basi hilo mmoja raia wa Tanzania na Botswana, huku abiria watano kati ya sita waliopakizwa kwenye lori nao wamepoteza maisha.
Raia wengine waliopoteza waliokuwa kwenye lori ni raia wa Ethiopia, Kenya, Zambia na wengine walibakia ni Watanzania huku juhudi za kufanya mawasiliano na balozi zao kwa utambuzi zikiendelea.
Taarifa hiyo inaodoa uvumi na taaruki iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii tangu jana usiku kwamba abiria 30 wamepoteza maisha kufuatia kutokea kwa ajali hiyo.
Taarifa hizo zimethibitishwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Mkombe Mkombe, huku akisema ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa tano Asubuhi baada ya lori hilo kupoteza uelekeo na kuhama njia na kwenda kuligonga basi hilo.
Hata hivyo, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mathew Mkingule amesema taarifa hizo amezipata, lakini kwa kuwa yupo likizo nchini, amewatuma wasaidizi wake kufuatilia kujua undani wa tukio hilo.
“Ni kweli taarifa nimezipata lakini sipo Zambia, nipo nchini kwa likizo. Kuna wasaidizi wangu nimewapa maelekezo wafuatilie kujua,” amesema Balozi Mathew.
Akizungumza kwa simu kutoka Afrika Kusini, mmiliki wa kampuni hiyo Mkombe, amesema wakati basi hilo linatoka lilikuwa na abiria 37 na wengi wao ni Watanzania.
“Basi wakati linatoka hapa Afrika kusini lilikuwa na abiria 37, sijajua kama njiani walipakia wengine lakini walipofika Zambia eneo la Sereje ajali ilitokea na madereva wetu wote wawili walipoteza maisha hapo hapo kwa sababu waligongana uso kwa uso,”amesema nakuongeza
“Chanzo ni dereva wa lori kuhama njia kulifuata basi na kusababisha kugongana uso kwa uso na watu zaidi ya 12 wamepoteza maisha na wengine majeruhi wamepelekwa vituo vya afya vya Sereje na Mkoshi maiti zipo Hospitali ya Mpika,” amesema Mkombe.
Amesema katika abiria hao saba waliopoteza maisha wakiwa kwenye basi, kuna mama mmoja raia wa Kenya ambaye ameacha mtoto mdogo mwenye umri unaokadiriwa kuwa na miaka minne.
Mkombe amesema, “Hana uhakika kama hadi inapata ajali hiyo walikuwa idadi hiyo inawezekana walipakiza wengine na unajua tena mambo ya madereva,” amesema.
Amesema kwa sasa wanachokifanya nikuwasaidia walionusurika na waliopata majeraha waweze kurudi nyumbani Tanzania huku akieleza tangu jana wanaendelea kuwatumia mahitaji mbalimbali ikiwemo fedha ya chakula.
“Sisi hatuja watelekeza tunawasaidia watu wote tofauti na kinachoelezwa kwenye mitandao,” amesema Mkombe.
Kwa upande wake mtumishi wa taasisi hiyo aliyeko Serenje ilipotokea ajali hiyo, Said Saad amesema kwa sasa yuko polisi anashughulikia nyaraka za watu waliopoteza maisha waweze kuwasafirisha.
“Kuwatambua watu ni changamoto kwa sababu waliokuwa kwenye lori hawajulikani tunaongeza umakini tusije tukasafirisha watu kuleta Tanzania kumbe ni raia wa Zambia au Wakenya,” amesema.
Amesema anachokifanya ni kwenda kuwachua Watanzania na Ubalozi wa Kenya nchini Zambia kusaidia kutambua miili hiyo kwa sababu imepelekwa sehemu mbili Mkoshi na Sereje.