Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

10 wauawa, maelfu wahama makazi yao shambulio la M23 DRC

DRC Yadai Rwanda Inafadhili Waasi Wa M23 10 wauawa, maelfu wahama makazi yao shambulio la M23 Mashariki mwa DRC

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kundi la waasi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) linalodaiwa kuwa na uhusiano na nchi jirani ya Rwanda limeuteka mji wa Nyanzale ulioko eneo la mashariki lililokumbwa na mapigano kufuatia mashambulizi yake yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 10 mbali na kusababisha maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.

Kwa mujibu wa Jonas Pandasi, kiongozi wa asasi ya kiraia katika eneo hilo, kutekwa kwa Nyanzale na waasi wa M23 kumejiri baada ya siku kadhaa za mapigano kati ya wapiganaji wa kundi hilo la waasi na vikosi vya usalama. Pandasi amesema, maelfu ya watu wamekimbia kuelekea Goma, ambao ni mji mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo DR na mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Kiongozi huyo wa asasi ya kiraia amebainisha kuwa, taarifa za awali zilisema idadi ya waliouawa ni karibu watu 10, huku nyumba zikiteketezwa kwa moto na maduka kuporwa bidhaa.

Aidha, hali ya kibinadamu imeripotiwa kuwa mbaya kutokana na karibu watu wote wa kijiji cha Nyanzale kuhama makazi yao na kukimbilia Kikuku. Raia wakihama makazi yao kunusuru maisha yao

Kwa mujibu wa Richard Moncrieff, Mkurugenzi wa Eneo la Maziwa Makuu wa Kundi la Crisis Group, kundi la waasi la M23 linadhibiti takribani nusu ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Ghasia na machafuko katika jimbo hilo zimezidi kuwa mbaya katika wiki za hivi karibuni huku vikosi vya usalama vikipambana na waasi. Wakazi wamesema wapiganaji wa kundi hilo mara nyingi hushambulia kwa mabomu kutoka kwenye vilima vinavyotazamana na miji ya mbali.

Mashariki ya Kongo DR ambayo iko mbali na mji mkuu Kinshasa, kwa muda mrefu imekuwa ikidhibitiwa na zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanayopigania kuwa na mgao wa madini ya dhahabu na rasilimali nyingine za eneo hilo huku yakifanya mauaji ya halaiki.

Matokeo yake ni kushuhudiwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ambapo takriban watu milioni saba wameyakimbia makazi yao, wengi wao wakishindwa kufikiwa na misaada.

Kundi kubwa katika eneo hilo la M23 lilipata umaarufu zaidi ya miaka 10 iliyopita wakati wapiganaji wake walipoiteka Goma, ambayo iko kwenye mpaka na Rwanda. Imepata jina lake kutokana na mkataba wa amani wa Machi 23, 2009 ambao unaituhumu serikali ya Kongo DR kwamba haikuutekeleza.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anadai kuwa Rwanda inaivuruga Kongo kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa nao pia wamewahusisha waasi hao na wanajeshi wa Rwanda, ingawa serikali ya Kigali inazikanusha tuhuma hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live