Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ziz Zag asimulia bao lililoiokoa Simba

Sun, 30 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Joto la mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga limeanza kupanda zikiwa zimebaki saa 48 kabla ya miamba hiyo ya soka kuteremka uwanjani kuwania pointi tatu muhimu.

Pia mchezo wa Simba na Yanga zinazotoka eneo moja la Kariakoo, jijini unatajwa wa kulinda heshima kutokana na historia ya klabu hizo.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umepangwa kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ambayo ndio mwenyeji wa mchezo huo, inahitaji ushindi ili kuendeleza ubabe kwa watani wao ambao wanataka kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa mwisho uliochezwa Aprili 29. Bao hilo lilifungwa na mchezaji kiraka Erasto Nyoni.

Mchezo huo wa Jumapili umemtoa ‘mafichoni’ aliyekuwa mshambuliaji hatari wa Simba, John Makelele ‘Zig Zag’ anayekumbukwa sana na mashabiki wa klabu hiyo.

Jina la ‘Zig Zag’ halitasahaulika kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa ndiye aliyefuta aibu ya timu hiyo kuteremka daraja mwaka 1988 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu).

Makelele akiwa katika ubora, alifunga bao la ushindi kwenye mchezo ambao Simba ilishinda mabao 2-1 Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na kuinusuru Simba kucheza mchangani kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo inayotoka Mtaa wa Msimbazi.

Ingawa mchezo wa Jumapili hauna madhara kwa Simba au Yanga, lakini nyota huyo ana kumbukumbu ya maandalizi ya mechi za watani wa jadi yanavyokuwa hadi siku ya mchezo.

“Mchezo wa Jumapili Simba na Yanga, unanikumbusha mbali, lakini kubwa zaidi tukio la mwaka 1988 nilipofunga bao la kuinusuru na janga la kuteremka daraja,”alisema Makelele anayeishi Babati mkoani Manyara akijishughulisha na kilimo, ufugaji.

Makelele aliyewika na Pamba ya Mwanza kabla ya kutua Simba mwaka 1988, anakumbuka mchezo dhidi ya Yanga ulivyokuwa na kila aina ya ushindani.

Nguli huyo alisema mchezo huo ulikuwa wa kufa au kupona kwa Simba kama ingefungwa au kutoka sare ya aina yoyote Simba ingeteremka daraja.

“Kimsingi sitasahau mechi ile katika historia yangu tulicheza na Yanga tukiwa tayari tumefungwa na Pamba bao 1-0 CCM Kirumba, viongozi wetu walikuwa na presha kubwa.

“Nakumbuka tuliweka kambi Dodoma wakati tukitokea Mwanza, viongozi walituambia kabisa jamani vijana wetu tumewapa dhamana ya kuibeba Simba lazima mshinde kwa njia yoyote ile,” anakumbuka Makelele.

Nguli huyo ambaye ni mwenyeji wa Songea, alisema siku ya mchezo walikula kiapo kila mmoja kucheza kwa juhudi na maarifa ili kupata ushindi dhidi ya watani wao.

“Mchezo ulikuwa mkali na Yanga iliingia uwanjani ikiwa na lengo la kutufunga, lakini tulipambana, Edward Chumila alifunga bao la kwanza na mimi nilifunga bao la pili la ushindi.

“Kuna baadhi ya watu wanadhani kipa Sahau Kambi alinirushia mpira kwa makusudi kama sehemu ya mbwembwe, hapana beki wetu wa upande wa kulia Raphael Paul alirusha mpira kutoka upande wa jukwaa la Yanga ukamparaza Chumila sasa wakati Sahau anataka kudaka ukamgonga, kama unavyojua enzi zile uwanja wetu haukuwa rafiki, ulipomgonga nikauwahi na kufunga,” alisema Makelele.

Hata hivyo, Makelele alidokeza ilikuwa shughuli pevu kupata ushindi kwa kuwa mabeki wa Yanga walikuwa hodari na alimtaja Godwin Aswile ‘Scania’ ndiye beki bora aliyekuwa akimuota siku zote wakati mchezo baina yao unapokaribia.

Pia Nguli huyo alimtaja Malota Soma ‘Ball Juggler’ ni mshambuliaji nyota aliyependa kucheza naye katika kikosi cha Simba na alimtaja beki wa kati Adolf Kondo, alikuwa akimvutia kati ya mabeki wa timu hiyo.

Makelele alitaja baadhi ya wachezaji waliocheza mchezo huo ni kipa Moses Mkandawile, Raphael Paul ‘RP’, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Adolf Kondo, Frank Kasanga ‘Bwalya’, Edward Chumila ‘Edo Boy’, Dan Muhoja, Makelele, Malota Soma na Sunday Juma.

Akizungumzia mchezo wa Jumapili, Makelele alisema Simba ina nafasi ya kushinda kwa kuwa ina kikosi kipana na amewataja Emmanuel Okwi na Meddie Kagera ni washambuliaji wazuri.

“Kimsingi ninaipa Simba nafasi ya kushinda, lakini mchezo wa timu hizi una maajabu yake,” alisema Makelele aliyepewa jina la Zig Zag na shabiki wa Pamba.

Makelele alianza kucheza soka ya ushindani Chuo cha Ushirika Moshi kabla ya kujiunga na Pamba na baadaye Simba alikocheza kwa mafanikio. Mchezo wa Jumapili utachezeshwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa kutoka Bukoba, mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Chanzo: mwananchi.co.tz