UKIACHANA na ushindi wlaioupata Yanga dhidi ya African Lyon wa bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid mshambuliaji wao Ibrahim Ajibu amesema hajafurahishwa na mchezo huo. Ajibu aliyeondolewa uwanjani dakika ya 86 nafasi yake ilichukuliwa na Said Juma baada ya mchezo huo alisema alitamani kufunga bao lake ambalo lingekuwa zawadi kwa kocha wake Mwinyi Zahera. Zahera hakuongozana na timu hiyo kwasababu yupo Uingereza kutatua matatizo ya kifamilia aliandaliwa zawadi hiyo na Ajibu kama ujumbe kwa kocha huyo kuwa mafundisho yake yanaeleweka. “Bao langu lilikuwa kiu yangu kubwa kuhakikisha namwambia mwalimu wangu kuwa mafundisho yake nimeyaelewa na nitayafanyia kazi kila siku hata asipokuwepo uwanjani ila nadhani presha ya ushindi na utelezi wa uwanja kutokana na mvua imepeperusha kabisa matumaini yangu,” alisema Ajibu Ajibu alikosa bao katika mashuti zaidi ya matatu ya mipira ya faulo aliyopewa kupiga na mwamuzi wa kati Eric Onoka, alisema anashangazwa na hali hiyo lakini haitamkatisha tamaa ya kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo. Kwa upande wa Mratibu wa klabu ya Yanga, Hafidh Salehe alisema kikosi chao kimecheza chini ya kiwango kutokana na uwanja huo kutelezi baada ya mvua kunyesha lakini ukosefu wa wachezaji sita tegemezi nao umechangia. Wachezaji waliokosekana ni Vincent Dante, Juma Mahadhi, na Thaban Kamusoko ambao wote ni majeruhi, Papi Shishimbi aliyeondoka kambini kutokana na matatizo ya kifamiliana Mrisho Ngasa mwenye kadi nyekundu na Feisal Totoo mwenye kadi tatu za njano.