Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zana: Wawa ameokoa kibarua changu Simba

46119 PIC+ZANA Zana: Wawa ameokoa kibarua changu Simba

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna mdau wa soka asiyefahamu umuhimu wa beki wa pembeni Shomari Kapombe katika kikosi cha Simba na Taifa Stars.

Uwezo wa kukaba na kufunga mabao, ulimtambulisha rasmi Kapombe kwa mashabiki wa soka hasa katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini, mbali na kucheza nafasi ya beki wa kulia, Kapombe ana sifa ya ziada ya kucheza nafasi ya kiungo na haikushangaza aliyekuwa kocha wa Simba Mfaransa Pierre Lechantre alimtumia katika mfumo 3-5-2.

Pia haikushangaza mashabiki wa Simba kupata na mshituko baada ya Kapombe kuumia walipopata taarifa za daktari kuwa atakuwa nje ya uwanja msimu mzima.

Mashabiki wa Simba walijiuliza beki gani anaweza kuvaa viatu vya Kapombe. Wapo waliomtaja Salum Kimenya wa Prisons ndiye mtu sahihi. Pamoja na matarajio ya wengi kwamba Simba itamsajili katika dirisha dogo, hali ilikuwa tofauti.

Mbelgiji Patrick Aussems alifanya uamuzi ambao awali ulitaka kumgharimu baada ya kumsajili Zana Coulibay raia wa Burkina Faso. Zana alisajiliwa kuwa mbadala wa Kapombe ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti.

Wadau wengi walimbeza Zana kutokana na kiwango chake alichokionyesha awali huku muonekano wake wa kuweka nywele rangi na makeke nje ya uwanja.

Hata hivyo Zana amewajibu mashabiki wa Simba waliokuwa wakimbeza kwa vitendo uwanjani. Kwasasa ndiye beki tegemeo wa kulia na tayari Kapombe ameanza kusahaulika.

Zana anamtaja beki wa kati Pascal Wawa ndiye amembakiza Tanzania kwa kuwa tayari aliona hana nafasi ya kucheza Simba na wakati wowote angetimuliwa.

“Wawa alinipa moyo alikuwa akiniambia hata yeye alivyokuja Tanzania mashabiki walibeza kiwango chake na kufikia hatua ya kumuita babu lakini hakujali alifanya kile ambacho kimemleta hapa Simba.

“Nilichukua maneno ya Wawa na kuyafanyia kazi jambo ambalo naamini limechangia kuniinua mpaka kufikia hatua hii, lakini sitaacha kushukuru ushirikiano wa wachezaji wenzangu bila wao pia nisingeweza kufika hapa,” anasema Zana.

Anasema wakati anafika nchini hakuwa fiti alikuwa na majeruhi ambayo yalimuweka nje ya uwanja muda mrefu.

“Mazoezi binafsi yananisaidia mpaka kufika hapa naamini bado kiwango changu ambacho kocha Patrick Aussems anakitambua sijakionyesha”anasema Zana.

Beki huyo anasema ana matumaini ya kufanya vyema katika Ligi Kuu kwa kuwa tayari ameanza kuzoea mazingira ya Tanzania.

Beki huyo mwenye mbwembwe, anasema anaamini Aussems ataendelea kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza baada ya kuonyesha kiwango bora.

“Namshukuru Aussems kuendelea kunipa nafasi ya kucheza licha ya wengi kuniona wa kawaida kwani bila yeye sidhani kama leo hii bado ningekuwepo Simba.

“Nitaendelea kufanya kile ambacho ananipangia katika mazoezi au mechi na kutimiza majukumu yangu kikamilifu,” anasema beki huyo.

Zana anasema hatabweteka na mafanikio ambayo ameanza kupata katika kikosi cha kwanza baada ya kumpoka namba Nicolaus Gyan.

Awali, Gyan alikuwa akicheza nafasi ya kiungo wa pembeni, lakini alirudishwa nyuma kucheza beki wa kulia kwa lengo la kuimarisha safu ya ulinzi.

Anasema anafurahia ushindani wa namba kwa kuwa utampa nafasi ya kuongeza kasi kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Zana anakumbuka mechi iliyomtoa ni ile dhidi ya Al Ahly ya Misri walioshinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Zana anasema mechi na Al Ahly ilikuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba.

“Mechi na Al Ahly nilijiona nimepewa dhamana kubwa jambo ambalo lilinifanya nicheze kwa nguvu ili kuisaidia timu yangu kupata matokeo mazuri.

Nakumbuka baada ya mchezo wachezaji wenzengu walinipongeza kwa kasi nzuri,” anasema beki huyo



Chanzo: mwananchi.co.tz