Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera sasa aipa Yanga dakika 90

39333 Zahera+pic Zahera sasa aipa Yanga dakika 90

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Yanga inacheza leo na Biashara United, morali ya wachezaji wa timu hiyo ipo juu na wameahidi kumaliza mechi hiyo ndani ya dakika 90.

Yanga na Biashara zinatarajiwa kumenyana katika mechi ya Kombe la FA, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini saa tatu hadi saa tano asubuhi jana, wachezaji walifanya mazoezi ya kutosha chini ya kocha Mwinyi Zahera.

Zahera alitoa maelekezo akiwataka wachezaji kucheza soka ya kasi, pasi tatu na kufanya mashambulizi haraka.

Mabeki Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’, Paul Godfrey na Gadiel Michael walipewa jukumu la kuanzisha mashambulizi na kuhakikisha mpira unavuka katikati kwenda kwa wapinzani.

Nahodha wa timu hiyo Ibrahim Ajibu alisema msingi wa mazoezi hayo ni kutaka kupata ushindi ndani ya dakika 90 kwa kuwa malengo yao siyo kufikia hatua ya kupigiana penalti.

“Inabidi tumalize mechi ndani ya dakika 90, hilo linawezekana kushambulia na kupata mabao ambayo yatatufanya tuvuke katika hatua hii na kusonga mbele,” alisema Ajibu.

Amissi Tambwe alisema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa Yanga imekuwa ikipata taabu kupata ushindi inapocheza na timu zisizokuwa na majina katika soka.

“Najua ugumu utakuwepo uwanjani, wapinzani wetu wanapokutana na Azam, Simba au Yanga wanakuwa tofauti. Hili huwa tunakutana nalo, hata hivyo tunataka tutoke na matokeo mazuri katika mchezo huu,” alisema Tambwe.

Akizungumzia mchezo huo, Zahera alisema ni muhimu kushinda ili kupata tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa na amewaandaa wachezaji wake kumaliza mechi ndani ya dakika 90.

“Hii ni mechi tofauti na ligi kwasababu ukipoteza unatoka, tunahitaji ushindi ndani ya dakika 90 ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika baadaye,” alisema Zahera.

Akizungumzia makosa waliofanya mabeki katika mchezo wa ligi ambao walifungwa bao 1-0 na Stand United, Zahera alisema amerekebisha kasoro hizo.

“Kweli kulikuwa na makosa katika michezo iliyopita hasa Sportpesa, lakini hata hivyo tumefanyia marekebisho ili kutatua tatizo hilo na kikubwa mashabiki wajitokeze kutushangilia,”alisema Zahera.

Pia Zahera alisema Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye anatarajia kurejea uwanjani Februari 8, atakuwa na msaada katika kikosi chake kwa kuwa ana nguvu ya kupambana.

Yanga inatarajiwa kucheza na Coastal Union, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Februari 2 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Katika hatua nyingine, Yanga imesema imepokea barua ya kipa Benno Kakolanya akitaka kuvunja mkataba na klabu hiyo. Kaimu Mwenyekiti wa Samwel Lukumay alisema wanatafakari barua hiyo kupitia wanasheria wao kabla ya kutoa uamuzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz