Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera kuvuta silaha matata

51714 ZAHERA+PIC

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WAKATI kikosi chake kikitarajiwa kushuka tena uwanjani jioni ya leo Alhamisi kuvaana na Kagera Sugar kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaambia Kamati ya kukusanya mabilioni ya usajili, anataka kabla ya msimu huu kufungwa avute silaha mbili mtata ili wasainishwe kukipiga Jangwani na fasta mabosi wake wakamwambia awashushe tu.

Mabosi hao wamemhakikisha Zahera kwamba silaha hizo mbili anazozitaka zije tu na wao watamalizana nao kwa sababu lengo lao ni kuona msimu ujao Yanga inakuwa tishio nje ndani.

Kikao cha Zahera na matajiri hao kilifanyika katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma wiki iliyopita na ndipo jambo hilo likaibuliwa na kocha huyo Mkongomani. Amewaambia mabosi wake kuwa katika kuonyesha hatanii anaposema anataka kusuka kikosi hicho na kushtua kwa kushusha vifaa hivyo.

Katika kikao hicho Zahera, amewaombea bajeti wachezaji hao wawili na kwamba wakitua tu wanatakiwa kusaini kisha kuwaonjesha burudani Wanayanga ili wachange haraka zaidi amalizane na wengine anaotaka watue.

Kocha Zahera ametaka vifaa hivyo vishushwe haraka kuwatia mzuka wanachama wake kuchanga zaidi katika mchakato wao wa kukusanya fedha lakini pia akiwawahisha wachezaji hao kutochukuliwa na timu nyingine.

Inaelezwa Zahera anayo majina ya nyota hao, lakini ameshindwa kuyaweka hadharani kwa sasa mpaka kwanza kila kitu kiwe sawa kwa kuhofia kilichomkuta kwenye dirisha dogo ambapo alipendekeza nyota kadhaa wakiwamo wa ndani na nje ya nchi, ila wote wakaishia kuja na kuondoka bila kusajiliwa.

Miongoni mwa wachezaji ambao Zahera aliwapendekeza na kuwataka wasajiliwe katika dirisha dogo ni Mganda Umaru Kasumba wa Sofapaka, Ruben Bomba kutoka DR Congo, kipa Farouk Shikalo wa Bandari Kenya na mshambuliaji machachari, Charles Ilanfya aliyekuwa Mwadui kabla ya kutua KMC, ila wote akawakosa na kujikuta akisajiliwa kipa Ibrahim Hamid na Haruna Moshi ‘Boban’ tu.

Ingawa haikuwekwa wazi, lakini Mwanaspoti limeambiwa kamati hiyo imemhakikishia Zahera kiasi cha 120 kumalizana na wachezaji hao wawili bajeti ambayo ilipitishwa haraka katika kikao hicho.

“Unajua kocha ameonekana amepania sana na ametaka kabla ya ligi kufungwa basi ashushe vifaa viwili vya maana ili watu watambue anachotaka kukifanya msimu ujao na kama kamati tumebariki uamuzi wake huo,” alifichua bosi mmoja.

Jeuri ya sasa ya Yanga ambayo Mei 5 itapata mabosi wapya kupitia uchaguzi wao mkuu, imetokana na Kamati hiyo kuweka mkakati ya kukusanya si chini ya Sh 1.5 bilioni, ambapo tayari wameshasambaza kadi 500 ambazo zina thamani ya Sh 500 milioni, mbali na michango inayoendelea kila uchao.

Kocha Zahera, alinukuliwa na Mwanaspoti hivi karibuni kuwa anataka kukijenga kikosi ambacho kitaweza kuhimili vishindo vya mechi za ndani na zile za kimataifa akiamini Yanga itabeba tiketi ya CAF kupitia ubingwa wa Ligi Kuu Bara ama Kombe la FA.

“Huwezi kushindana kama una kikosi dhaifu,” alisema Mkongomani huyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz