Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera apangua kikosi Yanga SC

40377 Pic+zahera Zahera apangua kikosi Yanga SC

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikiteremka uwanjani leo kuikabili Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha Mwinyi Zahera amesema atachukua uamuzi mgumu ili kupata ushindi.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Zahera alisema hana namna zaidi ya kupangua kikosi chake ili kupata matokeo mazuri katika mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Namfua, Singida.

Zahera alisema analazimika kufanya mabadiliko ili kuepuka muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha katika mechi mbili zilizopita.

Yanga ilionja shubiri baada ya kufungwa bao 1-0 na Stand United ya Shinyanga kabla ya Jumapili iliyopita kulazimisha sare 1-1 na Coastal Union ya Tanga.

Kocha huyo alisema sababu kubwa ya kupangua kikosi imetokana na ratiba ngumu iliyopo mbele yao aliyodai kuwa inawachosha wachezaji.

Alisema analazimika kuwapumzisha baadhi ya wachezaji kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kikosi chake ili kufanya vizuri katika michezo yote hasa ya ugenini. Zahera raia wa DR Congo, alisema anashangazwa na ukaribu baina ya mechi moja na nyingine huku wakitakiwa kusafiri umbali mrefu kucheza mechi za ugenini.

“Hii ni ajabu unacheza ligi unasafiri saa 15 njiani ili kucheza mechi nyingine. Haiwezekani mchezaji anacheza leo anasafiri umbali mrefu anapumzika siku moja na kesho anacheza mechi nyingine hawezi kuwa sawa,”alisema Zahera.

Kikwazo

Matokeo ya mechi mbili zilizopita dhidi ya Stand United na Coastal, yanaiweka Yanga katika mazingira magumu ya kupata ushindi katika michezo mitano ijayo ya ugenini.

Timu hiyo imecheza michezo 21 ikiwemo 10 ya ugenini, imeshinda saba, imepata sare mara mbili na kupoteza mmoja.

Msimu uliopita Yanga ilicheza michezo 15 ugenini, iliambulia pointi 18 baada ya kushinda mitano, sare mitatu na kupoteza mitano matokeo yaliyochangia kupoteza ubingwa mbele ya Simba.

Baada ya kucheza na JKT Tanzania Februari 10, Yanga itavaana na Simba Februari 16 na Februari 20 itaikabili Mbao Uwanja CCM Kirumba, Mwanza kabla ya kuifuata Namungo katika mchezo wa Kombe la FA.

Yanga na Alliance Machi 2 na Machi 10 itakuwa Dar es Salaam kucheza na KMC kabla ya kupepetana na Lipuli ya Iringa Machi 16.

Yanga imeifunga Singida United katika mzunguko wa kwanza mabao 2-0 wakati msimu uliopita zilitoka suluhu, pia zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa marudiano Uwanja wa Taifa.

Timu hizo zilikutana tena kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Namfua na Singida ilishinda kwa penalti 4-2 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

Kauli ya Mayay

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay amemtaka Zahera kurudisha ubora wa baadhi ya wachezaji wake muhimu katika kikosi ili kuipa uhai Yanga.

“Yanga katika mechi kama tatu au nne zilizopita ilishinda, lakini kiwango chao hakiridhishi kulikuwa na makosa mengi hasa safu ya ulinzi.

“Kama Zahera anataka ubingwa ahakikishe kwanza anarejesha ubora wa wachezaji wake muhimu kama Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu, Feisal Salum na Kelvin Yondani kabla ya kuanza kuwanyanyua wengine. Hawa ni wachezaji ambao wamekuwa wakiamua matokeo ya Yanga,” alisema Mayay.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga alisema suala la ratiba ni changamoto tangu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilipobadili ratiba ya mashindano yake na idadi kubwa ya makocha wamekuwa wakilalamika muda mfupi wa kujiandaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz