Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera ampa kazi maalumu Mwandila

14036 Pic+zahera TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mechi za kuwania kufuzu fainali za Mataifa Afrika mwakani, zimemlazimisha kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kubadili gia angani na kumpa jukumu zito msaidizi wake Noel Mwandila kuhakikisha timu yake haiathiriki na uwepo wa mechi hizo.

Kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kuinoa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zahera ataiacha Yanga kwa muda na kwenda kujiunga na kambi ya taifa lake inayojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Liberia, Septemba 9 huko Monrovia.

Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya DRC, alisema kipindi chote ambacho atakuwa akitimiza majukumu hayo, kibarua cha kuhakikisha Yanga inaendelea kuwa imara na kuimarika zaidi kitakuwa mikononi mwa msaidizi wake Noel Mwandila.

“Naondoka Agosti 30 kujiunga na kambi ya timu ya taifa ambayo itacheza ugenini dhidi ya Liberia, Septemba 9. Hata hivyo kuhusu Yanga nadhani kila kitu kitaenda sawa na programu zote zitakuwa chini ya usimamizi wa kocha Noel Mwandila.

Sidhani kama kukosekana kwangu kutaiathiri timu kwani sio mara ya kwanza kwangu kwangu kwenda kwenye majukumu ya timu ya taifa.” alisema Zahera.

Ratiba ya mechi kimataifa mara kwa mara imekuwa na athari kwenye programu za timu kutokana na kuondoka kwa wachezaji muhimu lakini pia wengine baadhi hupata majeraha wakiwa na timu zao za taifa jambo ambalo huleta wakati mgumu kwa makocha kukamilisha programu zao kwa asilimia 100.

Mfano wa hilo unaonekana kwa Yanga ambayo mbali na Zahera pia itawakosa Andrew Vincent ‘Dante’, Beno Kakolanya, Feisal Salum, Kelvin Yondani na Gadiel Michael ambao wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Wakati Yanga ikiwakosa wachezaji watano, Simba itawakosa wachezaji 10 ambao ni Haruna Niyonzima, Cletous Chama, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Erasto Nyoni, John Bocco, Shomary Kapombe, Aishi Manula, Shiza Kichuya na Hassan Dilunga.

Wakati Kapombe, Dilunga, Kichuya, Manula, Nyoni na Kapombe wakiitwa kwenye kikosi cha Stars, Okwi ameitwa kwenye kikosi cha Uganda, Chama (Zambia) huku Kagere na Niyonzima wakijumuishwa kwenye kikosi cha Rwanda.

Azam FC yenyewe itawakosa Tafadzwa Kutinyu aliyeitwa kwenye kikosi cha Zimbabwe, Nico Wadada (Uganda) na Yahya Zayd, Aggrey Moreis na Mudathir Yahya (Taifa Stars

Wakati huo huo, Ligi Kuu inaendelea leo kwa mchezo kati ya Simba na Mbeya City utakaoanza saa 10:00 kwenye Uwanja wa Taifa. Mchezo mwingine ni kati ya Alliance itakayocheza na African Lyon wakati Azam itakwaruzana na Ndanda.

Chanzo: mwananchi.co.tz