Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera alivyoibeba Yanga Ligi Kuu Bara

61248 Yangapic

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Klabu ya Simba imekabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Stand United na African Lyon zimeshuka daraja na msimu ujao zitacheza Ligi Daraja la Kwanza.

African Lyon ilimaliza ligi ikiwa na pointi 23 na Stand United ilishika nafasi ya 19 kwa pointi 44.

Katika mechi za mwisho African Lyon ilifungwa mabao 2-0 na KMC, Stand United ilitoka suluhu na JKT Tanzania.

Pia Kagera Sugar iliyoshika nafasi ya 18 kwa pointi 44 sawa na Mwadui iliyoshika nafasi ya 17 zitacheza mechi za mchujo ‘Play Off’ na timu mbili za Pamba na Geita zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza. Namungo FC ya Lindi na Polisi Tanzania, zimepanda Ligi Kuu.

Wakati Simba ikikabidhiwa kombe lake baada ya kutoka suluhu na Mtibwa Sugar, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ameacha alama kwa klabu hiyo kutokana na uhodari wake wa kuisemea kwa nguvu zote wakati wa mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Zahera alikuwa kivutio kwa wadau wa soka ambapo mbali na kufanya kazi yake ya ukocha, lakini alitumia muda mrefu kuipigania katika mambo mbalimbali.

Pia Soma

Kocha huyo alichukua jukuku jipya la kuwalea wachezaji wa timu hiyo katika kipindi chote cha mashindano hayo.

Mtikisiko wa kiuchumi ulioikumba Yanga, ulimuibua Zahera ambaye alianza kuipiga debe akitaka michango ya hali na mali ili kuhakikisha vijana wake wanarejea mchezoni.

Zahera raia wa DR Congo alikuwa akitoa fedha za mfukoni kusaidia wachezaji wake walipokuwa wakikabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi.

Yanga ilicheza mashindano hayo katika mazingira magumu na Zahera alibeba matatizo ya wachezaji bila kubagua.

Klabu hiyo ilianza kuyumba kiuchumi baada ya aliyekuwa mfadhili na mwenyekiti wake Yusuf Manji kujiuzulu.

Tangu Manji ajiuzulu, Yanga ilipitia kipindi kigumu baada ya kuyumba kiuchumi, hivyo Zahera alichukua jukumu la kutembeza bakuli kutaka michango ya wadau kuisaidia Yanga katika kampeni ya kutwaa ubingwa.

Zahera alifanya kazi kubwa kwa kuwa idadi kubwa ya wadau wakiwemo wabunge walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Yanga inapata fedha nyingi za kuwasaidia wachezaji.

Kocha huyo anasema hakuwa na namna ya kuhamasisha michango ya wadau wa klabu hiyo kwa kuwa aliamini Yanga ina idadi kubwa ya mashabiki nchini.

“Yanga ni klabu kubwa sana hapa Tanzania, lazima ishirikishe wadau wake waweze kuichangia ili wachezaji wapate stahiki zao,” anasema Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo. Pamoja na magumu yote iliyopitia Yanga, wachezaji wanastahili pongezi kwa kucheza kwa nguvu hadi dakika ya mwisho.

Chanzo: mwananchi.co.tz