Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera aing’ang’ania Yanga, jeuri yake ya fedha hii hapa

89251 Zahera+pic Zahera aing’ang’ania Yanga, jeuri yake ya fedha hii hapa

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

KAMA ni miongoni mwa watu waliokuwa wakijiuliza jeuri ya pesa kwa aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera (Papaa) inatoka wapi? Mchongo wote huko hivi.

Zahera tangu ametua Yanga hakuona shida kutumia fedha zake za mfukoni kuikopesha klabu hiyo ambayo sasa anaidai mamilioni ya fedha.

Kocha huyo ambaye hata baada ya kuvunjiwa mkataba na Yanga, hajaondoka nchini anakwambia hategemei mshahara wa ukocha, anapiga pesa kwa njia nyingine.

“Kila mmoja amekuwa akisema yake juu ya maisha yangu na kitu gani kinaniingizia fedha, lakini ukweli huko hivi, nafanya biashara Congo na Ufaransa,” anaanza kusimulia Zahera katika mahojiano maalumu na gazeti hili, huku akisisitiza anasubiria Yanga wampe chake kabla ya kwenda Zambia kuanza kupiga kazi nchini humo.

Kuhusu jeuri yake ya fedha, kocha huyo mwenye maneno mengi, anasema nchini Congo anamiliki hoteli ya kisasa inayoitwa Lavier Bier ambayo ina watumishi 41.

“Wote nawalipa mshahara, lakini pia Ufaransa nina ghorofa yenye orofa tatu ambayo nimeipangisha, hivyo ndivyo vitu vinaniingizia fedha,” anasema kocha huyo.

Anasema mbali na mshahara wa ukocha ambao alikuwa akilipwa na Yanga, kwenye timu ya taifa ya Congo fedha anayoingiza ni nyingi zaidi.

“Napenda tu kazi ya ukocha kwa kuwa ndiyo profesheni yangu, lakini si kazi ambayo ndiyo naitegemea ili niishi,” alisema.

Anasema alikuwa akitumia fedha zake za mfukoni kuikopesha Yanga kwani hakupenda kuona timu anayoifundisha inapata changamoto wakati anaweza kuitatua na baadaye wakarejesha fedha zake.

“Nilikuwa nikisaidia katika ndege, hoteli, posho na hata tulipokuwa Botswana kwenye mashindano ya kimataifa, nilitoa kulipia basi ambalo wachezaji walitumia kule.

“Kuna kiongozi (alimtaja jina) alitaka tutumie basi la wapinzani wetu kwa sababu hakuna pesa, wachezaji walishangaa, nikasema hapana hatuwezi kufikia huko, nikatoa pesa tukakodi basi lililobeba wachezaji kule,” anasema.

Timu gani atakwenda baada ya Yanga?

Zahera ambaye amehusishwa kujiunga na Namungo anasema timu atakayofundisha ni ile inashiriki mashindano ya kimataifa na si vinginevyo.

“Nitafundisha timu kubwa ambazo zinashiriki mashindano ya CAF (Afrika), lakini mimi kama kocha siwezi kukataa kuisikiliza timu yoyote ikitaka kuzungumza na mimi, ila ni ipi nitafundisha naamua mimi,” alisema.

Anasema tangu Yanga imetangaza kuvunja naye mkataba, timu nyingi zimemfuata zikiwamo za hapa nchini, lakini bado hajaamua ni ipi afundishe.

“Nimetumiwa tiketi na moja ya timu kubwa nchini Zambia, lakini kwa kuwa sijamalizana na Yanga, nimeshindwa kwenda,” anasema.

Kocha huyo anasema anachokisubiri Yanga ni malipo yake ambayo licha ya kutotaka kuyaweka wazi, lakini amesisitiza kuwa ni fedha nyingi.

Apanga kuanzisha akademia Bongo

Kocha Zahera licha ya kutoswa na Yanga, amesisitiza kwamba mpango wake wa kuanzisha kituo cha soka cha kisasa hapa nchini, upo palepale na kwa sasa anafanya utafiti ni eneo gani litamfaa.

Anasema eneo ambalo anahitaji kujenga akademi hiyo anataka liwe kubwa na liwe mita chache kutoka barabarani ili kuwapa urahisi wachezaji.

“Jambo lililonifanya nianzishe kituo cha soka hapa ni baada ya kugundua hakuna vituo vya kisasa, vingi havifuati utaratibu ambao unatakiwa. Nimewahi kuona vituo vingi vya soka vya hapa, unakuta wanawachanganya wachezaji wenye umri wa miaka tofauti 10, 11, 12, 13 na 15 wanacheza pamoja kitu ambacho si sahihi kwa mifumo ya soka,” anasema na kuongeza;

“Pia niligundua wachezaji wengi wa ligi kuu, unakuta wanatumia mguu mmoja wa kuume hawawezi kucheza wa kushoto sio kosa lao kwani hawajafundishwa misingi sahihi, lakini ikianzia chini itasaidia kuandaa kizazi chenye uwezo wa juu.”

Anaendelea kueleza anataka kuandika historia ya kuwatoa wachezaji wengi wa kucheza Ulaya kwa miaka ya baadaye ambao watakuja kuisaidia timu ya taifa kuwa na ushindani wa juu dhidi ya mataifa mengine.

“Mfano Senegal, Ivory Coast wana wachezaji wengi wanaocheza soka la Ulaya kwa sababu waliwaandaa wachezaji wao kwenye misingi sahihi ndio maana soka lao lipo juu, lazima tukubali kuanza chini.”

“Naona jambo hili linaungwa mkono na baadhi ya Watanzania kuna wale ambao wameniomba nikaangalie vituo vyao ili niviendeleze, kuna ambao walinipa kiwanja Mlandizi, bado sijaamua nifanye lipi kwa muda huu,” anasema.

“Kuna mawili chuo hicho kinaweza kuendelezwa nikiwa hapa ama Ufaransa, yote yanawezekana kikubwa ni vitendea kazi kuwepo.”

Awatofautisha wanasoka mastaa

Kwa uzoefu wake wa kuishi Ulaya na Afrika, kocha huyo ametofautisha wachezaji mastaa wa Ulaya aliowaelezea kwamba wana nidhamu na miili yao kwa sababu wanatambua kwamba ndio kitendea kazi kikuu.

“Staa wa Ulaya humkuti akilewa hovyo, wanajali sana miili yao kwani wanatambua wazi wakiichakaza biashara zao zinakuwa hazina thamani, wanakunywa ila kwa ustarabu,” anasema na kuongeza;

“Wanazingatia vyakula vinavyotakiwa, wanapumzika kwa wakati, sio watu wa kufanya starehe bila mpangilio kila kitu wanatenda kwa kiasi.”

Aliwaelezea mastaa wa Afrika kwamba ni watu ambao hawathamini miili yao, wanapopata pesa kidogo basi wanafanya starehe za kufifisha viwango walivyo navyo.

“Unakuta mchezaji anakunywa pombe za ajabu ajabu tena wanalewa, Ulaya unakuta staa anakunywa mvinyo tena grasi moja mbili, huku sasa ni kufuru.”

“Afrika mchezaji kuwa na wapenzi wanne, watano haoni shida, wakati mwingine wanapewa mapumziko wanadanganya wake zao kwamba wapo kambini, wengi hawajui thamani ya miili yao,” anasema.

Elimu na Soka

Zahera anasema kuna haja kwa wachezaji kuona umuhimu wa elimu anayoamini itawarahisishia kuelewa mambo kwa uharaka yanayoelekezwa na makocha wao.

“Yaani angalau wapate elimu kidogo itawasaidia sana kwenye soka, nimeliona hilo hii ni kwa Afrika na sio Tanzania pekee, ndio maana unamuelekeza hiki baada ya dakika tano anafanya mambo mengine, wakisoma watajua thamani yao ilivyo kubwa,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz