Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zahera ageuka turufu Jangwani

55758 ZAHERA+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati wanachama wa Yanga leo wakiwa na nafasi adhimu ya kuchagua uongozi mpya wa klabu hiyo, jina la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera limegeuka kuwa karata muhimu ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika leo jijini.

Umaarufu wa Zahera tangu alipotua Yanga, Aprili 2018 umekuwa ukiongezeka siku hadi siku huku akizidi kuwa kipenzi cha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutokana na tabia yake ya kuwa muwazi kuzungumzia changamoto zinazoikabili timu hiyo.

Lakini pamoja na hilo, Zahera ametokea kuteka hisia na nyoyo za mashabiki na wanachama wa Yanga kutokana na namna alivyo na ushawishi wa kuwajengea morali wachezaji ambao wamekuwa wakicheza kwa kujitolea licha ya hali ngumu ya kiuchumi ambayo timu hiyo inapitia, mbinu zake za kiufundi huku wakati mwingine akitoa zawadi ya fedha kwa nyota wake jambo lililoifanya timu hiyo iwe kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 80.

Kutokana na hilo, licha ya wagombea kuwa na sera na mipango yao ambayo wamekuwa wakiinadi, wengi wameamua kulitaja jina la Zahera mara kwa mara kwenye kampeni zao katika kile kinachoonekana kama njia ya kutengeneza ushawishi kwa wapiga kura.

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti, Mbaraka Igangula, alimsifu Zahera na kusema kuwa iwapo wanachama watamchagua, mambo mazuri yanakuja kwa kocha huyo.

“Mimi namsifu sana kocha, amefanya kazi nzuri licha ya nyakati ngumu ambazo klabu yetu imekuwa ikipitia. Huyu ni kocha anayepaswa kuungwa mkono na uongozi wangu utahakikisha unampa kila anachokitaka pindi tukiingia madarakani,” alisema Igangula.

Ni kama ambavyo mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Dokta Mshindo Msolla ambaye naye amekoshwa na kazi iliyofanywa na kocha huyo na kutamba kuwa atampa nguvu kubwa zaidi iwapo ataingia madarakani.

“Mimi ni kocha wengi wananifahamu labda atake ushauri tu wa kiufundi, nitaingia Yanga kama mwenyekiti tu, niseme wazi kuwa nitamwacha awe huru kutekeleza majukumu yake.

“Uongozi wangu hautakuwa na mipango ya kuachana naye, mara kadhaa nimekuwa nikisema wazi kuwa Yanga tuna bahati ya kupata kocha wa namna hii,” alisema Dokta Msolla.

Mgombea wa nafasi ya Umakamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela alisema atahakikisha Zahera anaongezewa majukumu na mamlaka na badala ya kuwa kocha, awe meneja kama ambavyo klabu za Ulaya na zile zilivyopiga hatua duniani zinavyofanya.

“Zahera ni zaidi ya mwalimu, baba katika timu yetu amekuwa akiishi nao vizuri na kuifanya timu yetu kupambana mpaka hivi sasa,” alisema Mwakalebela.

Naye Yono Kevela anayewania pia nafasi ya umakamu mwenyekiti alisema iwapo atachaguliwa kwenye nafasi hiyo, atamtengenezea Zahera mazingira bora na sahihi ya ufanyaji kazi.

“Kocha Mwinyi Zahera amekuwa kama yatima. Nikiingia madarakani kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nitamsaidia kwa kuweka mfumo endelevu wa kupata wachezaji bora na wenye viwango vya juu kuisaidia timu ya Yanga,” alitamba Kevela.

Winga wa zamani wa Yanga, Sunday Manara alisema kutajwa kwa Zahera kwenye kampeni za wagombea wengi wa nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo kunatokana na makubwa ambayo ameyafanya kwenye klabu hiyo.

“Ameleta ujasiri kwa mashabiki wa Yanga kutembea vifua mbele ndiyo maana amekuwa akitajwa kwenye kampeni.

“Ukimtazama Zahera unakuwa umeshika vichwa vya Wanayanga, tuna bahati Yanga kuwa na kocha wa kiwango chake,” alisema Manara.



Chanzo: mwananchi.co.tz